Madaktari Watakiwa Kuzingatia Maadili Ya Taaluma


WAMJW-Dodoma

Wanataaluma ya Udaktari wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni Na Maadili ya taaluma hiyo katika utendaji kazi wao kama inavyoainishwa katika kifungu cha Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi.

Hayo yamesemwa jana na Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika Dkt. David Mnzava alipokuwa anaongea na waandishi wa Habari jijini Dodoma.

Dkt. Mnzava amesema kumekuwa na uvunjifu wa Sheria kwa baadhi ya wanataaluma kwa kukiuka Kanuni za Madaktari, Madaktari wa Meno na wanataaluma wa Afya Shirikishi, hivyo amewataka kuzingatia sheria hizo.

Sheria ya mwaka 2017 inasimamia utendaji Kazi wa kada ya Udaktari, Udaktari wa Meno, Wataalamu wa mazoezi ya tiba, Wataalamu wa viungo bandia, Wataalamu wa Magonjwa ya Akili na utengemao, Matabibu, Matabibu Wasaidizi na Wataalamu wa Meno wasaidizi.

Aidha Dkt. Mnzava amesema Uvunjwaji wa Kanuni hizi utasababisha kosa la Kimaadili kama inavyonukuliwa katika kifungu cha 41 (2).

“Kifungu hicho kinasema Mtaalamu wa Udaktari, Udaktari wa Meno au Afya Shirikishi ataonekana kukosa sifa ya kutoa huduma, chini ya Sheria hii atakuwa amekiuka Sheria za Maadili.” Amesema Dkt. Mnzava.

Hata hivyo Baraza limetoa wito kwa wasimamizi wa Mikoa na Wilaya kuweka mipango thabiti ya kusimamia utendaji wa wanataaluma katika maeneo yao



from MPEKUZI

Comments