Upatikanaji wa maji wafikia 67% Simiyu


Samirah Yusuph,

Itilima.
Hali ya upatikanaji wa maji kwa mkoa wa Simiyu imefikia asilimia 67.5 ikilinganishwa na miaka miwili nyuma upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 40.5 huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 85 ifikapo 2023.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila  Octoba 29,2021 alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani Itilima mkoani hapa   na kusema kuwa  zaidi ya wananchi milioni 1.05 wananufaika na maji safi na salama.
 
Amesema katika kipindi cha miezi sita ilyopita mkoa umepokea kiasi cha Sh10.8 bilioni ili kuboresha na kukamilisha miradi ya maji na kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

"Ni uhakika kuwa kwa miaka miwili ijayo tatizo la maji litakuwa limepungua na upatikanaji wa maji kuwa kwa asilimia 85 ambapo robo tatu ya vijiji vyote vitakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji".

Mkoa wa Simiyu unajumla ya wakazi 1,584, 157 kwa mujibu wa sensa wa mwaka 2012 huku ukiwa na jumla ya vituo 4380 vya kuchotea maji (DP's)ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vituo vya kuchotea maji vilikuwa 2948.

Amesema upatikanaji wa maji katika mkoa wa Simiyu unategemea vyanzo vya maji vya asili na visima vilivyo chini ya Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini ambapo ni visima virefu 35 vilivyokamilika na 36 vikiwa katika hatua ya mwisho ya ukamilishaji pamoja na visima vifupi vilivyo chimbwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf.

Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Itilima wameelezea hali ya upatikanaji wa maji kwenye wilaya hiyo na kusema kuwa hali ya upatikanaji wa maji bado sio nzuri sana kwa sababu visima vilivyopo havijitoshelezi.

"Baadhi ya maeneo wanapata maji ya uhakika lakini kuna maeneo hakuna maji kabisa na wanategemea mito, mabwawa visima vya chini ambavyo vinakuwa ni vya msimu wa mvua pekee" Alisema Edward Mwandu mkazi wa Itilima.

"Bado tunaamka usiku kutafuta maji hasa hasa msimu wa kiangazi, kwa kuwa serikali italeta mitambo ya kuchimba visima tunaomba vijiji ambavyo havina maji kabisa vipewe kipaumbele" Alisema  Matha Ezran mkazi wa Itilima.

Mbali na Mpango huo wa kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji pia Mkoa wa Simiyu unatarajia kuanza ujenzi wa mradi wa kusafirisha maji kutoka ziwa viktoria wenye thamani ya zaidi ya Sh400 bilioni.

Ambao linatarajiwakuwa na urefu wa kilomita 194 na kufikia vijiji 244 pamoja na hilo pia serikali imetoa mtambo mmoja kwa ajili ya kuchimba visima kila Mkoa na mtambo mmoja wa kutengeneza mabwawa kila kanda.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments