Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Abdallah Chaurembo ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi na kutatua kero zinazowakabili pindi wanapohitaji huduma katika taasisi za umma.
Mhe. Chaurembo ametoa pongezi hizo leo wakati wa kikao kazi cha kamati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika katika Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.
Mhe. Chaurembo amesema, kamati yake inaridhika na utendaji kazi wa Ofisi hiyo hasa katika kubuni mifumo ya TEHAMA inayosaidia kuondoa malalamiko ya wananchi.
Mhe. Chaurembo amesema kamati yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuwasisitiza wajumbe wa kamati yake kutoa elimu ya matumizi ya mifumo hiyo kwa wananchi wanapokuwa kwenye maeneo yao ya utawala.
“Mambo mazuri sana yamefanywa na Ofisi hii pamoja na taasisi zake, hasa hili la kubuni mifumo ya TEHAMA inayoondoa malalamiko, hivyo wajumbe wa kamati hii tuwasaidie kutoa elimu ya umuhimu wa mifumo hii kwa wananchi, tuwasisitize wananchi watumie mifumo hii kuondoa malalamiko,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.
Akitoa neno la utangulizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, Serikali kupitia wataalam wa ndani wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imekuwa ikibuni mifumo mbalimbali kwa lengo la kusogeza huduma za Serikali karibu na wananchi na kuwaweka wananchi karibu na Serikali yao.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa Ofisi yake iliona ni vema kufanya ubunifu wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma na wananchi kwa kipindi cha muda mrefu.
Akifafanua jinsi mfumo mmojawapo uliobuniwa na wataalam hao ujulikanao kwa jina la Sema na Waziri wa UTUMISHI unavyofanya kazi, Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huu unamuwezesha mwananchi kuwasilisha kero au lalamiko lake moja kwa moja kwake na kulifanyia kazi.
Mhe. Mchengerwa amewaomba Wajumbe wa Kamati ya USEMI kutoa elimu ya faida za mfumo huu kwa watumishi na wananchi katika maeneo yao ili utumike kutatua changamoto zinazowakabili.
“Mkiwa kama wawakilishi wa wananchi, tunaomba mtusaidie kupeleka ujumbe kwa wananchi kuhusu faida za mfumo huu kwani tunataka kupunguza kabisa malalamiko na kutatua changamoto za kiutumishi zinazowakabili Watumishi wa Umma kwa muda mrefu.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa ameishukuru kamati kwa kuiongoza na kuishauri vema ofisi yake na kuahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na kamati hiyo kwa maslahi ya taifa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Ndomba amesema Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kimelenga kwenye ubunifu na utafiti katika TEHAMA ili kuwa na mifumo itakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhandisi Ndomba amesema falsafa ya Kituo hicho ni kutumia wataalam wa ndani katika kujenga mifumo hiyo ya TEHAMA ili kuweza kutatuta matatizo yetu wenyewe.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment