Jeshi lachukua mamlaka kamili Sudan, hali ya hatari yatangazwa


Jeshi la Sudan limevunja serikali ya mpito iliyokuwa inajumuisha raia na wanajeshi na wakati huo huo kuwakamata viongozi wa kisiasa akiwemo waziri mkuu na kutangaza hali ya hatari nchi nzima.

Jenerali Abdel Fattah Burhan, ambaye alikuwa akiongoza baraza la pamoja na viongozi wa kiraia, ametoa tangaza hilo na kusema mapinduzi ya sasa ya kijeshi yamesbabaishwa na malumbano ya kisiasa.

Amedai kuwa jeshi limelazimika kulinda usalama wa nchi kwa mujibu wa katiba na kuongeza kuwa mbali na serikali ya mpito kuvunjwa  magavana wote wa majimbo nao wamefutwa kazi na kwamba uchaguzi utafanyika Julai 2023.

Kufuatia uamuzi huo wa jeshi, waandamanaji wenye hasira  wamemiminika  kwenye barabara za mji mkuu, Khartoum na kuwasha matairi barabarani huku milio ya risasi ikiendelea kusikika katika jiji hilo.

Viongozi wa jeshi na raia wamekuwa wakizozana tangu kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir kupinduliwa miaka miwili iliyopita na serikali ya mpito kuanzishwa.

Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ni miongoni mwa viongozi wa kiraia ambao wamezuiliwa nyumbani. Chama cha wanataaluma cha Sudan ambacho ni mwamvuli wa vyama vya wafanyakazi ambavyo vilikuwa muhimu katika maandamano ya mwaka 2019 ya kumpinga Bashir, kimeshutumu kile walichokiita "mapinduzi ya kijeshi" na kuwataka waandamanaji kupinga vikali hatua hiyo.

Ripoti zimebaini kuwa mawasiliano ya mtandao yamekatishwa na kwamba jeshi na vikosi vya kijeshi vimepelekwa kote jijini Khartoum. Aidha uwanja wa ndege wa Khartoum sasa umefungwa, na safari za ndege za kimataifa zimesimamishwa.




from MPEKUZI

Comments