Cyprian Musiba aamuriwa na Mahakama kumlipa Benard Membe Bilioni 6


 Mahakama Kuu ya Tanzania, imemuamuru Mmiliki wa Gazeti la Tanzanite, Cyprian Musiba kumlipa Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe kiasi cha Sh.Bilioni 6 kama fidia ya kumchafua kupitia vyombo vyake vya habari.

Hukumu hiyo ya shauri la kesi namba 220 ya mwaka 2018 imetolewa na Jaji Joacquine De Mello ambapo amesema mbali na mambo mengine Musiba amlipe Sh.Bilioni 6 Membe, pia inatoa zuio la kudumu la kutomkashifu Membe au kusema uongo dhidi yake na kulipa gharama za kesi.

Mahakama imesema Sh.Bilioni 5 ni fidia ya hasara halisi na Sh. Bilioni 1 hasara ya jumla.

Katika kesi hiyo Membe alimshtaki Musiba, Mhariri wa gazeti la Tanzanite na wachapishaji wa gazeti hilo ambapo aliwadai Sh. Bilioni 10 kwa kumchafua.

Musiba katika kesi hiyo alishtakiwa kwa kumtuhumu Membe kuwa anamhujumu Rais John Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo huku akidai kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020 kupitia CCM.


from MPEKUZI

Comments