Aveva ahukumiwa kifungo miezi sita, Kaburu aachiwa huru


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfunga kifungo cha nje cha miezi sita aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi huku Godfrey Nyange maarufu Kaburu akiachiwa huru baada ya mahakama hiyo kutomkuta na hatia

Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba ambapo amesema hakuna ubishi wowote kuwa Dola za Kimarekani 300,000 zilikuwa zimeingizwa kwenye akaunti ya Klabu ya Simba kupitia benki ya CRDB ambayo ni mauzo ya mchezaji Emanuel Okwi

Alisema baada ya kuingia kwenye akaunti hiyo inaonyesha kwamba kamati tendaji ya klabu ya Simba ilielekeza itolewe fedha hiyo kwenye akaunti ya Simba ili itumike kwenye uwanja wa Bunju kujenge nyasi bandia.

“Mahakama imejitosheleza kuwa ile fedha ilitakiwa ijenge nyasi bandia kwenye uwanja wa Bunju lakini haikufanyika hivyo matokeo yake zilienda kwenye akaunti binafsi ya Aveva,” Simba

Alisema mahakama hiyo imejiridhisha kuwa mashtaka yote hayajadhibitisha isipokuwa shtaka la matumizi mabaya ya ofisi ambalo  ni kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Klabu ya Simba na kwenda akaunti binafsi.

Hakimu Simba alisema kutokana na mashtaka hayo Nyange amekutwa hana hatia isipokuwa Aveva amekutwa na hatia kwa kutumia nafasi yake vibaya kwa kuingiza fedha hizo kwenye akaunti binafsi ingawa hakuna wizi uliofanyika.

“Hela zote zilitumika kihalali isipokuwa tatizo lake hizo fedha ziliingizwa kwenye akaunti binafsi” Simba.

Baada ya maelezo hayo Wakili wa Serikali, Fatma Waziri alidai hawana kumbukumbu ya makosa ya jinai yaliyotendwa na mshtakiwa huyo hivyo anaiomba mahakama itoe adhabu Kali ili iwe funzo kwake na Kwa wengine wanaotumia madaraka vibaya ya ofisi.

Naye Wakili wa utetezi, Kuge Wabeya aliieleza mahakama hiyo kosa lake ni la kwanza kwa mshtakiwa, pia ni mgonjwa amekuwa akihudhuria Kliniki mara tatu kwa wiki na ana familia inayomtegemea.

“Tunaomba itoe adhabu nafuu itakayowezesha kuhudhulia kliniki na wakati akiwa anasubiliwa mshtakiwa alikaa mahabusu tangu mwaka 2017 Hadi mwaka 2020,” Wabeya.

Hakimu Simba alisema kutokana na mazingira yaliyopo ya kesi amezingatia hoja za pande zote mbili kuwa mtuhumiwa amekaa mahabusu kwa muda mrefu mpaka pale mahakama ilipoona kosa la utakatishaji halijathibitishwa.

“Kumpeleka gerezani kwa maana kumfunga haitasaidia chochote kwani watakuwa wamemfunga mgonjwa ambaye itakuwa imesababisha usumbufu siyo kwa mshtakiwa bali hata magereza na jamii Kwa ujumla,” Simba.

“Hata ukimpiga faini kubwa bado haitasaidia chochote kwani asipolipa atalazimika kupelekwa gerezani hivyo adhabu pekee inayomfaa mahakama imeona atumikie kifungo cha nje miezi Sita na asifanye kosa lolote,”alisema

Simba alisema rufaa ipo wazi kwa yeyote kama hajaridhika na maamuzi hayo

Katika kesi ya msingi, Aveva anadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.


from MPEKUZI

Comments