Aliyekuwa Msaidizi wa Lengai Ole Sabaya atoa ushahidi kesi ya Freeman Mbowe na Wenzake

Shahidi wa pili upande wa Jamhuri katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Justine Eliya Kaaya ametoa ushahidi.

Kaaya, ambaye alikuwa mpiga picha wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ametoa ushahidi huo Jumatano Oktoba 21, 2021 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Akiongozwa na Wakili Chavula, Kaaya amedai alianza kufanya kazi kwa Sabaya mwaka 2017 kama mpiga picha hadi 2018 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Kilimanjaro alipokuwa msaidizi wake, ikiwemo kumpelekea chakula ofisini kwake.

Kaaya amedai kuwa, Oktoba 2018 aliondoka nyumbani kwa Sabaya alikokuwa anaishi naye mkoani Kilimanjaro na kurudi nyumbani kwake Longido mkoani Arusha.

Shahidi huyo wa Jamhuri amedai, Novemba 2018 alipokea simu kutoka kwa Mbowe akimtaka waonane lakini alisitia kwa kuwa alikuwa na hofu kwani hakuwa na mahusiano naye kabla.

Kaaya amedai, baada ya kusita Mbowe aliamua kumfuata mwenyewe mkoani Arusha, ambapo walionana majira ya saa tatu usiku ndani ya uwanja wa mpira uliko mji Mdogo wa Longido, na kuingia katika gari yake.

Kaaya amedai, baada ya kuingia ndani ya gari, Mbowe alimwambia Ole Sabaya anamsumbua sana pale Hai na kuwa yeye ni mtu wake wa karibu, na kumtaka ampe taarifa za shughuli anazofanya na watu aliokuwa nao.

Amedai, Mbowe alimuambia kuwa yeye ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani hivyo atafanya namna yoyote anavyoweza kumrudisha kwa sabaya ambapo amesema alimjibu akisema hawezi kwa kuwa aliamua kufanya shughuli zake binafsi.

Kaaya amedai, baada ya kutoa kauli hiyo, Mbowe alimpa Sh.300,000 akisema ni za usmbufu na kwamba baada ya hapo waliagana akaondoka.

Amedai baada ya Mbowe kuondoka alimpigia simu sabaya ili ampe taarifa lakini hakupokea simu. Ndipo akampigia simu Mbunge wa Longido, Dk Steven Kiruswa kumueleza kilichotokea.

Kaaya amedai, mwanzoni mwa 2020 Mbowe alimpigia simu kwa mtandao wa Whatsapp, akimtaka waonane amfuate Moshi kwa kuwa yeye alikuwa Arusha.

Akiongozwa na Wakili Chavula, Kaaya amedai baada ya wito huo alipanda usafiri wa Costa kuelekea Moshi.

Hii ni sehemu ya ushahidi aliotoa Kaaya

Shahidi: Naitwa Justine Eliya Kaaya, nafanya kazi za kilimo cha mbogamboga yaani nyanya, vitunguu na viazi mbatata

Wakili Chavula: Taratibu jaji asikie

Hebu rejea nafaka unamaanisha nini

Shahidi: Mahindi na maharage, nazifanyia Wilaya Arumeru Arusha. Mwaka 2017 nilikuwa naishi Wilaya ya Longido mkoa wa Arusha. Nilikuwa nashughulika na upigaji picha na pia kilimo Arumeru

Wakati huo nilikuwa nimelima karoti na mahindi. Wateja wangu walikuwa ni kutoka masokoni.

Upigaji picha nilikuwa napiga picha za mnato. Nilikuwa nawapigia viongozi wa Serikali na wa kisiasa

Viongozi hao walikuwa Dk Steven Lemomo Kiruswa, mbunge wa Longido. Mrisho Mashaka Gambo aliyekuwa RC Arusha, Gabriel Nyagaro aliyekuwa DC Arusha mjini na wengine. Serikalini alikuwemo Lengai Ole Sabaya.

Sabaya mara kwanza nilikutana naye 2017 katika uchaguzi mdogo Longido. Wakati huo alikuwa Diwani Kata ya Sambasha, Arumeru na alivutiwa upigaji wangu wa picha

Sabaya alinitaka nikamsaidie kazi hiyo na shughuli nyingine mbalimbali ndani katika kata yake.

Nilimkubalia kwa sababu ilikuwa ni fursa kwangu. Nilihama Longido kwenda Arusha, nyumbani kwa Sabaya Kibanda Maziwa, Sakina.

Nilikuwa nikiishi na Sabaya na mkewe na nilifanya naye kazi hadi mwaka 2018 Julai alipoteuliwa kuwa DC Hai, nilikwenda kuishi naye katika makazi ya DC Hai, Kilimanjaro.

Hapo nilikuwa msaidizi wake katika shughuli ndogo ndogo Kama kumpelekea nguo zake Dry Cleaner, chai na chakula ofisini kila siku.

Hapo niliishi na  Sabaya na mkewe na mwezi Oktoba, 2018 niliamua kurudi Longido kuendelea na majukumu yangu mengine, sababu niliacha mchumba na nilitaka nikasimamie shughuli zangu za kilimo.

Mwezi Novemba 2018 siku moja jioni nikiwa nyumbani nilipigwa simu kwa namba yangu ya airtel 0693006700 na namba ya Airtel 0784779944 na mtu aliyejitambulisha kama Freeman Mbowe. Kwanza nilishtuka kwani sikuwahi kuwasiliana naye.

Aliponipigia aliniuliza hujambo nikamwambia sijambo akasema nina shida ya kukuona ni muhimu sana. Nilimuuliza mahali aliko akanijibu yuko Arusha. Nikamwambia niko Longido na nina changamoto ya usafiri.

Aliniambia chukua gari Noah nitakuja kulipa gharama baada ya wewe kufika Arusha.

Lakini, kwa sababu ya ile hofu nilimwambia sitakuja kwanza ni kiongozi mkubwa simfahamu na sina ukaribu wowote na yeye.

Aliniambia subiri nakupigia akakata simu na baada ya muda alinipigia tena akaniambia niko njiani nakufuata Longido.

Kwa sababu alishaniambia yuko njiani anakuja nilishindwa kumzuia nikasema acha nimsubiri nisikie anachotaka kuniambia.

Baada ya dakika 40 alinipigia tena simu akaniambia njoo hapa uwanja wa mpira Longido.

Nilimuita bodaboda anipeleke pale, nikakuta gari liko pale linaunguruma na muda huo ilikuwa ni saa 3 usiku.

Nikimpigia simu kwenye namba ileile  ya 0784779944, akaniambia sogea kwenye gari. Nikasogea akashusha kioo cha dirisha akaniambia ingia kwenye gari chief usiwe na wasiwasi. Nikamruhusu yule  boda akaondoka nami nikafungua gari mlango wa nyuma nikaingia.

Alikuwemo yeye na upande wa dereva alikuwepo mwanamke. Aliniambia kwamba Lengai anasumbua sana pale Hai na mimi mi mtu wake wa karibu. Akawa anataka nimpe taarifa ya shughuli anazofanya na watu  ambao yuko nao pale Hai. Nikamwambia haitawezekana kwa sababu mimi sipo tena na Sabaya.

Aliambia yeye ni kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani kwenye nchi hii, hivyo atafanya namna yoyote atakayoweza nirudi kwa Sabaya niendelee na kazi. Nilimwambia haitawezekana sababu nimechagua kufanya kazi zangu binafsi.

Aliniambia samahani kwa kukusumbua na alinipa Sh300,000, nikamuuliza ni za nini akaniambia ni za usumbufu. Tutawasiliana. Tuliagana akaondoka

Niliposhuka kwenye gari nikampigia Lengai simu nimpe taarifa, lakini hakupokea simu. Niliendelea kusimama pale uwanjani na baadaye nilimpigia mbunge wa Longido, Dk Steven Kiruswa kumweleza habari hizo. Nilimuita boda boda nikarudi nyumbani.

Mwanzoni mwa mwaka 2020, alinipigia tena simu kwa mtandao wa WhatsApp kwa namba ileile baada ya salamu aliniambia tumepotezana sana Chief, aliniambia anataka tuonane, nimfuate Moshi wakati huo mimi nilikuwa Arusha. Nilimwambia niko shambani kumwagilia nikishamaliza nitakuja.

Baada ya shughuli zangu nilipanda Coaster nikampigia simu kumpa taarifa kwamba ninakwenda.

Baada ya kumpa taarifa aliniambia nishuke Machame Road, Wilaya ya Moshi mkoni Kilimanjaro.

Baada ya kufika nilishuka kwenye gari na kumpigia simu kwa namba yake ileile ya Airtel. Aliniambia nisubiri hapo anakuja.

Baada ya muda akanipigia simu akaniambia nimefika umekaa upande upi nikamwambia nimekaa upande wa kushoto  akaniambia njoo upande wa kulia. Kuna njia ya Machame na nyingine ya Arusha.

Nilipofika nikakuta gari V8 nyeusi yenye mlingoti na bendera ya Bunge yenye plate number za KUB.

Ilisimama karibu yangu ikashusha kioo cha upande wa abiria na hapo nikamuona mwenyekiti Freeman Mbowe akaniambia panda. Alishuka mtu kutoka kwenye kiti cha abiria nyuma akaniambia pita.

Tuliendelea kuzungumza ile gari ilichukua uelekeo wa Machame, baada ya dakika kama nane iliingia mahali ni Hotel ya Aishi.

Ndani ya gari kulikuwa na dereva na huyo mlinzi wake aliyenipisha nikaingia kwenye gari. Nilikuwa sifahamiani nao.

Aliyenipisha nilijua ni mlinzi wake baada ya kunitambulisha kuwa ni mlinzi wake Kanda ya Kaskazini na pia ni Diwani wa Kata ya Kibororoni.

Ile hotel nilitambua kwa sababu niliona kibao kilichoandikwa Aishi Hotel.

Baada ya kushuka kwenye gari mimi, Mbowe na yule mlinzi wake, tulienda kuketi upande wa mgahawa, akaniambia kuwa tutazungumza kwa muda mfupi kwa sababu ana mikutano ndani ya jimbo.

Aliniambia niagize kinywaji au chakula. Muda huo ilikuwa saa 7 mchana na simu ya kunitaka tukutane alinipigia saa 2:30 asubuhi.

Safari ya kuelekea Moshi kutoka Arusha niliianza saa 5 kasoro asubuhi na nilianzia sehemu inatwa Kilala wilayani Arumeru.

Kwanza Mbowe aliuliza kuna mipango gani juu ya hii mikutano ninayoifanya jimboni nikamwambia sijui chochote kinachoendelea. Aliniambia nimtajie majina ya wasaidizi wa Sabaya anaotembea nao, nilimwambia sina taarifa yoyote ya kumweleza. Nilimtajia yale majina na yule Diwani akawa anayaandika kwenye karatasi, majina ya Japhet Lwendela, Vedastus Sigula, Mtoto wa Mkulima, Sylvester Nyegu, Binti wa Kichaha, mwalimu Doreen na Watson Malimungu.

Akaka na namba zao za simu, nikazitaja wakaziandika akasema atashughulika nao tutawasiliana mimi na yeye baadaye.

Baada ya mazungumzo Freeman Mbowe aliniaga kuwa anakwenda kwenye mikutano na kwamba, baadaye atanitumia chochote kwenye simu yaani nauli. Alitimiza ile ahadi lakini hakunitafuta baada ya pale. Baada ya pale nilirudi Arusha.

Mwezi wa 7 2020, Siikumbuki tarehe alinipigia kwa namba yake ya Airtel kwa njia ya mtandao wa WhatsApp namba ya 0784779944, aliniambia niko njiani natoka Dar naomba jioni tuonae nina jambo la muhimu kuzungumza na wewe uje Moshi. Wakati huo nilikuwa shambani kwangu na ilikuwa mchana saa 8.

Niliendelea kufanya shughuli zangu ilipofika saa 11 jioni nilianza safari ya kwenda Moshi, nilipanda basi la Kiumbocharo liliokuwa likitoka Singida. Aliniambia kuanzia saa 1 usiku atakuwa amefika Moshi. Nilishuka Moshi stendi saa 1:30 usiku.

Nilimpigia simu namba yake ileile nikamwambia nimefika., aliniambia nichukue pikipiki nimfuate Kizo hotel mjini Moshi.

Nilichukua bodaboda nikamwambia nipeleke Kizo hotel nilipofika nikampigia Mbowe simu  0784779944 nikamwambia nimefika. Aliniambia namtuma msaidizi wangu akufuate. Baada ya muda alikuja dereva wake ambaye namkumbuka kwa jina moja la Willy, sababu tulipokutana mara ya kwanza Machame ndiye  alikuwa anamwendesha.

Tulikwenda nyuma ya hotel ambako kuna swimming. (Willy) aliniambia Mheshimiwa yuko kwenye kikao, hivyo tukae hapa tumsubiri amalizie kikao.

Japo tulikuwa na mlinzi wake ambaye alikuwa baunsa kidogo, ambaye Willy aliniambia kuwa nisiwe na wasiwasi. Tulikula yule mlinzi wake alielekea alikokuwa Mbowe baada ya muda mfupi alirudi akasema tunaondoka.

Aliniambia (Freeman Mbowe) pole sana kwa kukuweka, yule mlinzi wake alinifungulia mlango wa gari na yeye mwenyekiti aliingia na nyuma aliingia aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Joyce Mukya nikakaa katikati na upande wa nyuma, Mbowe akakaa mlinzi wake.

Baada ya pale kutoka Kizo hotel gari ilielekea uelekeo wa Arusha mpaka Aishi Hotel Machame.

Baada ya kushuka kwenye gari akamwambia yule mbunge atangulie ndani sisi tuna kikao kifupi.

Tulikaa upande wa mgahawa, Mbowe, mlinzi wake, dereva alipotaka kujumuika akimwambia hiki kikao ni cha watu watatu wewe kaa pembeni hakikuhusu.

Alinitambulisha akiniambia yule ni mlinzi wake na msiri wake anaitwa Halfan Bwire hivyo niwe huru kujumuika naye.

Huyo mlinzi tulikuwa tumekaa naye mkono wake wa kushoto.

Aliniambia nimtajie tena majina ya wale wote watu wa Sabaya na namba zao za simu na kazi wanazozifanya kwa Sabaya. Kabla sijaanza kumtaja alimwambia mlinzi wake yule Halfani Bwire achukue kalamu na karatasi ili aandike. Baada ya kurudi aliniambia nimwandikie. Hivyo nilianza kuandika majina na namba za simu.

Wale walikuwa ni marafiki zake na Sabaya ambao nilikuwa nawafahamu na namba zao za simu nilikuwa nazo kwenye simu maana tulikuwa tunafahamiana.

Majina aliyoandika ni yale ya mwanzo nyongeza ni Enock Kirigiti.

Baadaye alinitaka nimtajie mahali Sabaya anapenda kutembelea, nilimtajia.

Baada ya kutoa taarifa hizo nikimuuliza mwenyekiti hizi simu unataka za nini? Akaniambia hilo niachie mimi kazi yako hapa imeisha.

Baada ya pale aliniambia nimkabidhi Halfani Bwire yale majina,  Halfani akasema huyu Sabaya ni mtu mdogo sana nitamchezesha.

Baada ya pale mwenyekiti aliniambia kazi imeanza rasmi kuanzia sasa hivi nitakuwa nakulipa mshahara.

Muda huo ilikuwa ni saa 4 usiku. Baada ya pale alisema utapewa chumba ulale hapa utaondoka asubuhi . Sababu sikuweza kupata usafiri kwenda Arusha ikibidi nilale pale. Asubuhi Ile alinitumia Sh200,000 kwa 0754916666 kutoka namba yake ya Airtel, airtel money 0784779944.

Kulipokucha nilirudi Arusha saa 12 asubuhi kuendelea na shughuli zangu za shambani.

Hatukuweza kuonana tena kwa sababu Agosti 25, 2020 nilikamatwa na Jeshi la Polisi.

Nilikamatwa Makumira wilaya ya Arumeru nikiwa naenda benki ya CRDB kupeleka hela.

Nilkuwa napeleka fedha baada ya kuuza mazao ya karoti ambayo nilikuwa nimewauzia watu wa Mount Meru. Nilikuwa na Sh1,117,000 Dola 1,100 za Marekani na Euro 240.

Niipokamatwa nilipelekwa Kituo Kikuu cha Arusha na baada ya saa moja nikaenda kupekuliwa nyumbani kwangu kisha nilisafirishwa kuletwa Dar es Salaam.

Zile pasa zangu zilichukuliwa na askari wakasema ni noti bandia. Waliniambia nina tuhuma za kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi.

Nilipofikishwa Dar nilipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam nikafanyiwa mahojiano na Afande Mahita. Niliwekwa ndani hadi nilipokuja kufikishwa Mahakamani Kisutu na kusomewa mashtaka mbalimbali ikiwemo, kushiriki vikao vya ugaidi, kula njama za ugaidi, kesi ya utakatishaji fedha na nikaunganishwa na wenzangu ambao tayari walikuwa gerezani watatu: Halfan Bwire, Mohamed Ling'wenya na Adamu Kasekwa.

Halfani Bwire kabla ya kuunganishwa naye nilikuwaga naye Kizi Hotel na Aishi Hotel akiwa na Mheshimiwa Mbowe.

Mohamed Ling'wenya nilikuwa simfahamu ndio ilikuwa mara ya kwanza na Adamu Kasekwa nilikuwa simfahamu pia.

Baada ya kuunganishwa kwenye kesi hiyo Kisutu nilipelekwa Gereza la Ukonga. Hapo nilikuwa na Halfan Bwire, baadaye akaletwa Khalid Athuman na baadaye akaletwa Mohamed Ling'wenya kutoka Segerea.

Nimekuwa kwenye kesi Ile kwa miezi 11. Julai 26, 2021 jioni aliletwa Mheshimiwa Mbowe gerezani Ukonga akanikuta na Halfan Bwire akasema poleni sana nimekuja kuwatoa.

Tulilala na ilipofika asubuhi watu wa Magereza walikuja wakasema jiandaeni kupelekwa mahakamani. Kesho yake Julai 27, 2021 tulipelekwa mahakamani watatu, mimi mshtakiwa wa nne, Khalid Athuman wa sita na Gabriel Mhina. Wakili wa Serikali alisema baada ya upelelezi kukamilisha hakuna ushahidi tukafutiwa mashtaka.

Zile Fedha zangu nikienda Mahakama Kisutu nikapelekwa Central nikakuta Mkaguzi Msaidizi Swila akaniandika maelezo ya uhusiano wangu na nilivyofahamiana na Mhe. Mbowe, baada ya muda nilipewa vitu vyangu vyote.

Mbowe, Halfani Bwire, Mohamed Ling'wenya na Adamu Kasekwa kwa sasa wako hapa mahakamani.

Wakili wa Serikali Chavula anamtaka shahidi awaonyeshe kwa majina na shahidi anawasogelea na kuwataja kwa majina huku akiwasonda kwa kidole akianza na Halfan Bwire, Adamu Kasekwa, Mohamed Ling'wenya na Mbowe. Kisha anarejea kizimbani.

Wakili: Mheshimiwa kwa sasa ni hayo.

Credit: Mwananchi



from MPEKUZI

Comments