Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji


Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Emmanuel Msomba (30) baada ya kupatikana na kosa la mauaji ya msafiri mmoja aliyekuwa akitoka Tunduma kwenda Sumbawanga mkoani Rukwa baada ya kumpiga na mti na kumpora fedha na simu ndogo aina ya Itel.

Uamuzi wa hukumu hiyo ulitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer, baada ya kusikiliza mashahidi zaidi ya wanane wa upande wa Jamhuri na kuridhika.

Hakimu Laizer alisema ushahidi huo ulieleza kwa kina kwamba mshtakiwa Msomba akiwa na wenzake wawili huko Kijiji cha Chiwanda, wilayani Momba, walimuua Isack Kazuka wakati akiendesha pikipiki kutoka Tunduma kwenda nyumbani kwao Kalambo, mkoani Rukwa.

Alifafanua kuwa marehemu Kazuka aliombwa lifti na mshtakiwa ambaye alishirikiana na wenzake kutekeleza mauaji hayo na kisha kumpora fedha na simu ndogo aina ya Itel baada ya pikipiki ya marehemu kudaiwa kuharibika.

Kwenye utetezi wake mshtakiwa Msomba alikana kutenda mauaji hayo badala yake alidai kuomba lifti ya pikipiki kwa Kazuka na aliachana naye kwa fundi wa pikipiki alikokuwa akitengeneza pikipiki yake hadi aliposikia mtu huyo amekutwa na umauti na kuiomba mahakama kumwachia huru kwa madai hakuhusika na mauaji hayo.

Licha ya upande wa utetezi kuomba kupunguziwa adhabu kwa mteja wake Jamhuri kupitia wakili Davice Msanga, kwenye utolewaji hukumu hiyo iliisihi mahakama kutoa adhabu kama sheria inavyoelekeza kwa kuwa bado watu wengi wanaendekeza uhalifu mbalimbali ikiwamo kukatisha maisha ya wenzao kwa tamaa za fedha na mali nyingine badala ya kufanya kazi kwa bidii na kumtanguliza Mungu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer kwa mamlaka ya nyongeza kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya baada ya kusikiliza mashauri ya mauaji, alimhukumu mtu huyo kwenda kunyongwa hadi kufa baada ya mahakama yake kuthibitishiwa mshtakiwa kumuua msamaria huyo aliyekatishwa maisha kijijini Chiwanda Momba wakati akielekea mkoani Rukwa.

Credit:IPP



from MPEKUZI

Comments