Waziri Mkuu: Sekta Ya Viwanda Imechangia Kuondoa Umasikini Nchini


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema sekta ya viwanda ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 23, 2021) baada ya kuzindua Upanuzi wa Kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL) tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

“Duniani kote, sekta hii imekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali na ndiyo mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuongeza thamani ya mali ghafi, kutoa ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni, kuongeza na kuboresha teknolojia.”

Amesema kwa kulitambua hilo, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta za viwanda kwa kuboresha miundombinu muhimu na wezeshi kama reli ya uhuru, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ili iweze kuchukua mizigo mizito na kuisafirisha kwa haraka kutoka sehemu moja hadi nyingine.

“Tumeongeza ufanisi wa utoaji mizigo bandarini sambamba na huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia za anga, maji na barabara. Hatua nyingine ni uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye upatikanaji wa nishati ya gesi, umeme wa uhakika, unaotabirika na kutosha mijini na vijijini.”

Amesema ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme wa maji la Mwalimu Nyerere, litakalozalisha umeme MW 2,115 una lengo la kuhakikisha tatizo la nishati ya umeme linabaki kuwa historia. “Uwepo wa bwawa hili, utasaidia siyo tu kuwa na umeme wa uhakika na ziada bali pia kuwa na umeme wa bei rahisi ambao utachochea uwekezaji wa viwanda.”

Ametoa wito kwa wawekezaji na wazalishaji kuchangia katika juhudi zinazofanywa na Serikali kuondoa changamoto zinazoathiri ukuaji wa sekta ya viwanda kwa kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora wa juu na kwa bei shindani ambayo hata mlaji wa kawaida atamudu kununua bidhaa hizo.

“Pamoja na kuwahimiza wazalishaji kuongeza ufanisi katika uzalishaji, pia ninapenda kuwasihi ndugu zangu Watanzania kupenda kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini. Kwa lugha nyingine tupende vya kwetu! Kwa kufanya hivyo, tutaongeza wigo wa soko la bidhaa za viwanda vyetu na kuviwezesha kukua na kuajiri vijana wengi zaidi.”

Amesema Serikali kwa upande wake, itaendelea kununua bidhaa zinazotokana na viwanda vya ndani katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kielelezo na kimkakati. “Tumeshatoa maelekezo kwa taasisi zetu kununua sare zao za nguo na viatu, mabomba ya maji na gesi, mabati, nondo, saruji kutoka katika viwanda vya hapa nchini.”

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara iendelee kuhamasisha wizara au taasisi za umma na binafsi zinunue na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili viwanda viendelee kuzalisha, kutoa ajira kwa vijana na pia Serikali itakusanya kodi na kuendelea kutoa huduma za jamii kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuwezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Amesema uwepo wa viwanda nchini kikiwemo na cha SBL ni soko muhimu kwa mazao ya kilimo kwa sababu zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wao wanatumia malighafi zinazotokana na mazao ya kilimo kutoka maeneo mbimbali nchini, ambapo wamepanga kuongeza na kufikia asilimia 85.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, Mark Ociiti alisema wametumia shilingi bilioni 13.4 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya upauzi wa kiwanda hicho na tayari wameanza kuzalisha pombe kali inayoitwa BONGO DON. “Awamu ya pili ya upanuzi wa kiwanda hiki inayotarajiwa kuanza hivi karibuni itagharimu shilingi bilioni 124.”

Mkurugenzi huyo alisema kampuni hiyo ina jumla ya viwanda vitatu katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro na wameajiri watumishi wa kudumu 800. Amesema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na ushirikiano inaowapatia katika kuhakikisha uwekezaji huo unakuwa na tija.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments