Waziri Jafo Atoa Siku 45 Kuteketeza Shehena Ya Kontena Za Mifuko Ya Plastiki


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo ametoa siku arobaini na tano kwa wataalamu wa Bandari, TRA, TBS na NEMC kwa Pamoja kushirikiana kwa mujibu wa sheria kuteketeza kontena za mizigo ya mifuko ya plastiki iliyopo bandari kavu ya Ubungo jijini Dar es salaam.

Ameyasema hayo alipofanya ziara katika bandari kavu ya Ubungo jijini Dar es salaam na kusema kuwa kuna kontena za mifuko ya plastiki kadhaa zimeingia na mizigo hii imetelekezwa hapa bandarini na kwa mujibu wa sheria ya Mazingira, mizigo hii inatakiwa kuteketezwa,

‘’Juni 2019 Serikali ilipiga marufuku matumizi ya mifuko hii ya plastiki kwahiyo natoa siku arobaini na tano kwa vyombo vyote kushirikiana kusimamia zoezi la kuteketeza kontena za mifuko ya plastiki iliyo kinyume na Sheria ya Tanzania na Uharibifu huu utasimamiwa na watu wa Mazingira NEMC. Lakini jambo lingine ni kwamba tusiruhusu bidhaa ambazo hazikubaliki ndani ya nchi yetu kuingizwa, lakini pia nipate ripoti ya kimazingira ni kwa jinsi gani kazi hii imefanyika.’’ alisema Waziri Jafo

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria NEMC, Bw. Benard Kongola amesema kuwa waliletewa taarifa kuna wadau wanaomba kununua kontena zilizo bandarini kusafirisha nje ya nchi kwasababu zilikamatwa zikiwa na mifuko ya plastiki ambayo haikidhi viwango vya kutumia nchini.

‘’Kwa mujibu wa kanuni ya plastiki ya mwaka 2019 ya mazingira inapiga marufuku ungizwaji, usafirishwaji nje ya nchi na uhifadhi wa nchini wa plastiki ambazo hazikidhi viwango. Kwa taarifa za TRA kontena hizi ziliingia mwaka jana mwishoni na zilikuwa zinaenda nchini Malawi. Sheria inakataa kuzisafirisha nje ya nchi itaonekana Tanzania ndo inasafirisha.

Naye Meneja wa TRA Bandari Bw. Fales Mniko amesema makontena yaliingizwa ikiwa utekelezaji wa sheria ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki umeanza,

‘’Makontena haya yaaliingizwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nchi nyingine na hatuwezi tukayauza kwasababu Sheria ya Mazingira imezuia, kwahiyo hizi kontena zimeingia kwenye listi ya utaratibu wa kuharibiwa.’’



from MPEKUZI

Comments