Simbachawene Asema Watanzania Wanataka Amani, Maendeleo, Siyo Katiba Mpya


Na Felix Mwagara, MoHA, Kibakwe.
WAZIRI wa Mambo ta Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema uimara wa Katiba ya Tanzania umeleta amani, kupendana, kushirikiana na kuwepo kwa kasi ya maendeleo nchini hivyo hakuna umuhimu wa kuwepo kwa mchakato wa Katiba mpya kwasasa, na vyama vya upinzani wanaitaka si kwa ajili ya wananchi bali kwa malengo yao binafsi.

Amesema hakatai kuwa Katiba inaweza kuwa na mapungufu kwa baadhi ya vipengele, hivyo vyama vya upinzani wanapaswa kusema eneo lipi lifanyiwe mabadiliko kama lipo na siyo kutaka katiba nzima ibadilishwe wakati bado ina ubora wa hali ya juu na ndiyo imeleta maendeleo makubwa nchini.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Makose na Chogola, Kata ya Masa, Jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, leo, Waziri Simbachawene amesema sekeseke na vurugu nyingi za vyama vya upinzani ni kuzungumzia katiba ambayo haina kosa lolote, na shida kuu ya wananchi ni vitu vya maendeleo na siyo Katiba.

“Unakuta mtu anaisema Katiba mbaya kwa kipengele kimoja tu cha Tume ya Uchaguzi, baasi, lakini Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyotuweka katika hali ya kupendana, nchi ya amani, Katiba hii ya Tanzania ndio inayopelekea Watanzania wanamiliki rasilimali na maliasili kwa umoja bila kuwa na ugomvi, nchi nyingine kila siku wanapigana mapanga kwasababu rasilimali za nchi zao zimewekwa katika mazingira ambayo Katiba yake haijaweka vizuri na watu wanagombana kila kukicha,” alisema Simbachawene.

Simbachawene aliongeza kuwa, Katiba ya Tanzania ni nzuri na hakuna kitu ambacho hakikosi mapungufu hivyo mapungufu ya hapa na pale yanaweza yakawa yapo na yanapaswa kushughulikiwa na siyo kwa kuibomoa Katiba yote, vinaweza vikachukuliwa vipengele muhimu vikarekebishwa kwa vile ambavyo  vinavyopigiwa kelele.

“Shida ya watanzania siyo Katiba mpya, ila shida ni yawanaotaka madaraka kwa njia nyepesi ndiyo shida yao wanaona ni Katiba, shida ya Katiba ni ya watu wachache tu kwa malengo, kwa ubinafsi wao lakini Tanzania hakuna shida ya Katiba maana Katiba hii ni nzuri na imetupitisha katika vipindi muhimu na vigumu ambapo ingesababisha nchi iweze kuvunjika,” alisema Simbachawene.

Ameongeza kuwa, katika mkutano wake na wananchi hao wameyataja masuala mbalimbali ya maendeleo wanayoyataka jimboni humo ikiwemo wanahitaji maji, zahanati, barabara nzuri, shule kujengwa zaidi, nyumba za walimu na madaktari lakini hawakusema wanataka Katiba mpya, hivyo siyo shida ya wananchi zaidi ya kutaka maendeleo.

Aidha, Waziri Simbachawene aliwataka wananchi wa Kata Masa kuhakikisha wanatunza mazingira kwakutokata miti, kuharibu vyanzo vya maji, na kusababisha barabara, mashamba, madaraja kuharibika kutokana na maporomoko ya maji kutoka milimani baada ya baadhi ya wananchi kuharibu mazingira hayo.

 “Afisa Mtendaji wa Kata nakuagiza hakikisha unalinda misitu, wachukulie hatua kali wanaokata miti, wanaolima milimani, nipo tayari nikose kura zao kwa wale ambao wanasababisha uharibifu wa mazingira, jamani kutunza mazingira ni muhimu, lazima mlijue hili, msifanye mzaha, mazingira yetu yanaharibika kutokana na wachache ambao wanalima na kukata miti kwa ajili ya kuchoma mikaa na shughuli zingine sio halali, jambo ambalo linaharibu mazingira yetu,” alisema Simbachawene.

Simbachawene amemaliza ziara jimboni kwake kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.


from MPEKUZI

Comments