Majaliwa Amsimamisha Kazi Afisa Manunuzi Wilaya Ya Karagwe


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Afisa Manunuzi wa Wilaya ya Karagwe Bw. Yesse Kaganda baada ya kutoridhishwa na viwango vya ubora wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karagwe ambayo imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5.

“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kila wakati anasisitiza usimamizi mzuri wa fedha zinazotolewa ili zitumike kwa ukamilifu na kujenga miradi yenye ubora, vigae hivi havijaanza kutumika tayari vimechakaa, Afisa Manunuzi huyu akae pembeni kwanza na vigae vipya viwekwe kwa gharama zake.”

Waziri Mkuu amesema Rais Mheshimiwa Samia ametoa pesa za kujenga na kukamilisha miradi ya maendeleo na kuhakikisha Serikali inasogeza huduma zote muhimu za kijamii lakini watendaji wachache wamekuwa wakishindwa kufuata maadili ya kazi zao na kujenga miradi isiyokuwa na ubora.

Ameyasema hayo jana(Jumapili, Septemba 19, 2021) baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera akiwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi mkoani Kagera.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa Mikoa na Wilaya wahakikishe wanasimamia vyema matumizi ya fedha zilizotolewana Rais Mheshimiwa Samia katika kutekeleza miradi ya maendeleo na huduma za jamii ili kuleta tija na mabadiliko kwa wananchi.

“Malengo ya Rais wetu sasa yanaenda kutimia kwani anataka kila mwananchi apate huduma za afya hukohuko aliko, kuanzia ngazi ya kijiji tunajenga zahanati na baada ya kuwa zahanati za kutosha tunajenga kituo cha afya ambacho kina huduma zote muhimu, kama upimaji wa magonjwa yote, chumba cha upasuaji, jengo la mama na mtoto pamoja na wodi za wanaume na wanawake”. Alisema

Waziri Mkuu amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Karagwe kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo utakamilika kwa wakati na kwa viwango kwani tayari fedha za kununua vifaa tiba vyote na mitambo ya mionzi zimetengwa.

Amesema wananchi pia wana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutoa maoni kwani miradi hiyo inatekelezwa kwa kodi za wananchi. “Ninawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na Serikali yenu pamoja na viongozi wake,”



from MPEKUZI

Comments