Maafisa 21 wakamatwa kuhusiana na jaribio la mapinduzi Sudan


 Jeshi la Sudan limetoa taarifa likisema kwamba maafisa 21 na wanajeshi kadhaa wamekamatwa kuhusiana na jaribio la mapinduzi lililotokea jana asubuhi na msako unaendelea kuwakamata wengine waliobakia waliohusika na tukio hilo. 

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa jeshi ambaye ni mshauri wa masuala ya habari, Brigedia Jenerali Altahir Abu Haja, jeshi limeyadhibiti tena maeneo yote yaliyokuwa yamekamatwa wakati wa jaribio hilo. 

Aidha serikali ya mpito ya nchi hiyo imesema wanajeshi na raia waliohusishwa na jaribio hilo wanafungamanishwa na utawala ulioondolewa wa kiongozi wa muda mrefu, aliyeongoza kwa mkono wa chuma, Omar al-Bashir. 

Waziri Mkuu Abdalla Hamdok amesema jaribio hilo ni njama za hivi karibuni za kuchochea mgogoro wa kitaifa, akigusia mgawanyiko mkubwa uliopo Sudan wakati ikielekea kwenye demokrasia. 

Akihutubia kupitia Televisheni amesema waliopanga njama hiyo walifanya maandalizi ya kina ambayo yamejionesha kupitia mapungufu ya kiusalama yaliyoonekana mijini, kufungwa kwa barabara, bandari na uchochezi uliokuwa ukiendelezwa dhidi ya serikali ya kiraia.



from MPEKUZI

Comments