Serikali Yaendelea Kutoa Elimu Kwa Wananchi Kuhusu Matumizi Ya Tiba Asili Nchini.

 Na WAMJW- DOM
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imeendelea na zoezi la kutoa Elimu kwa wananchi katika maeneo ya kutolea huduma za Afya juu ya umuhimu wa matumizi ya tiba asili/mbadala katika mapambano dhidi ya magonjwa mbali mbali, ikiwemo UVIKO-19.

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya tiba asili ya mwafrika Wadau wa tiba asili wakiongozwa na kitengo cha Tiba asili na Baraza la tiba asili kutoka wizara ya afya wameweza kutembelea na kutoa elimu katika  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma, kituo cha Afya cha Makole na Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

Akiongea wakati wa utoaji elimu hiyo Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili/Mbadala  Dkt. Vumilia Liggyle alisema kuwa, Wataalamu wa Tiba asili na tiba mbadala kutoka Wizarani wameongozana na Waganga wa tiba hizo kutembelea vituo vya Afya katika sehemu ya wagonjwa wa nje wa Hospitali (OPD) ambapo wameweza kuzungumza na wagonjwa na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa tiba asili katika mapambano dhidi ya magonjwa mbali mbali nchini.

"Kwa siku ya leo tumetembelea vituo vya Afya vitatu, tumetembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma General kama kituo cha kwanza, ambapo tumeenda sehemu ya wagonjwa wa nje wa Hospitali ambapo tumeweza kuzungumza na wagonjwa na kuwapa elimu kuhusu tiba asili." Alisema.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali tuna Baraza la tiba asili na tiba mbadala ambalo linatekeleza Sheria namba 23 ya mwaka 2002 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza hili ndio linasajili dawa, Waganga wa tiba asili, na kuwajua wako wapi na wanafanya nini, na kuhakikisha dawa hizo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Baraza la tiba asili na tiba mbadala linafanya kazi kwa kushirikiana na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya TMDA, maabara ya taasisi ya dawa asili pamoja na Maabara ya Shirika la viwango Tanzania, Alisisitiza Dkt. Liggyle.

Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la dawa asilia na ulinzi wa mazingira Bw. Boniventura Mwalongo ameeleza zaidi ya asilimia 93 ya dawa zinaagizwa kutoka nje ya nchi, hivyo Serikali imelenga kuboresha tafiti za ndani, kuongeza uzalishaji wa ndani ili kutoa fursa za ajira, hususan kwa vijana, hivyo kupitia kuikuza tiba asili nchini yote yanawezekana.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Waganga wa tiba asili katika zoezi hilo Dkt. Elizabeth Lema alisema kuwa, wiki hii ya maadhimisho inatoa fursa kwa Waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuonesha bidhaa zao mbali mbali ambazo tayari zimesajiliwa kupitia Baraza la tiba asili na tiba mbadala na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuhudhuria maonesho hayo yatayofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ili kujifunza, kuelimishwa na kupata fursa ya kuuliza maswali mbali mbali kuhusu tiba asili na tiba mbadala kisha kufahamu namna ya kuzipata na kuzitumia.

Wiki ya tiba asili na tiba mbadala ya Mwafrika inaongozwa na Kauli mbiu ya "Mchango wa tiba asili katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 " ambapo mwisho wa kilele ni Agasti 31, huku Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kufunga maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka.



from MPEKUZI

Comments