Jerry Silaa Ajisalimisha Kamati Ya Maadili ya Bunge Kabla Ya Kukamatwa

 Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa amefika katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhojiwa baada ya jana Kamati hiyo kutoa ombi kwa Spika wa Bunge Job, Ndugai kutaka akamatwe.

Kamati hiyo iliomba kukamatwa kwa mbunge huyo na kufikishwa katika kikao cha kamati saa 4.00 asubuhi leo Ijumaa Agosti 27,  2021.

Silaa aliitwa kuhojiwa kwa mara ya kwanza katika kamati hiyo Agosti 24, 2021 akituhumiwa kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

Imedaiwa kuwa Silaa alifika saa 12.00 asubuhi leo katika viwanja vya Bunge, eneo ambalo lina kinga ya kukamatwa na vyombo vya dola kwa mujibu wa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

Hata hivyo, kabla ya kuitwa kuingia katika kamati hiyo, Silaa alikwenda moja kwa moja katika ukumbi wa Spika ulioko jengo la Utawala la Bunge akiwa pekee yake bila kusindikizwa na askari kama ilivyokuwa Agosti 24, 2021 alipohojiwa kwa mara ya kwanza.



from MPEKUZI

Comments