Viwanja 594 Vyapimwa Kuzunguka Hospitali Ya Kanda Ya Kusini

 


Na Munir Shemweta, MTWARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema Wizara yake imepima viwanja 594 katika eneo linalozunguka hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kusini na kumilikishwa kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika hospitali ya Kanda ya Kusini uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Isdor Mpango leo tarehe 26 Julai 2021, Dkt Mabula alisema, pamoja na ujenzi wa Hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa huduma za kitabibu, wizara ya Ardhi  iliona umuhimu wa kupima viwanja eneo hilo na kumilikisha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi na shughuli nyingine.


“Mhe Makamu wa Rais pamoja na ujenzi wa hospitali hii uliofanywa na Shirika letu la  nyumba la Taifa, wizara imepima na kumilikisha jumla ya viwanja 594 kuzunguka hospitali hii ili kuwezesha wananchi kujenga nyumba za makazi na shughuli nyingine” alisema Dkt Mabula.


Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, NHC imekuwa ikifanya kazi nzuri katika miradi mbalimbali na ujenzi wa hospitali ya Kanda ya kusini itakayohudumia mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi ni moja ya miradi mikubwa ya kimkakati iliyotekelezwa na shirika hilo.
Dkt Mabula alisema, mradi mwingine wa kimkakati unaojengwa na shirika la NHC ni ule wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyopo eneo la Kwangwa sambamba na miradi ya ujenzi wa  nyumba na ofisi za Wakala wa huduma za misitu (TFS).


Aidha, Naibu Waziri Mabula alimuomba Makamu wa Rais kulisaidia Shirika kupatiwa miradi ya ujenzi na Taasisi za Serikali kwa kuwa Shirika hilo kwa sasa liko imara na linao uwezo wa kujenga miradi ya ujenzi iliyo na ubora wa hali ya juu.


Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango  alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa ujenzi wa jengo hilo alilolieleza kuwa lina ubora usio na mashaka.


Alizitaka Taasisi za Serikali zenye miradi ya ujenzi kutoa kupaumbele kwa NHC katika ujenzi wa miradi yake na kulitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuzingatia ubora wakati wa utekelezaji miradi sambamba na  kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na vifaa vya ujenzi kwenye miradi hiyo vinatoka nchini Tanzania.


Alilitaka shirika la Nyumba kukamilisha ujenzi wa mradi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kwa wakati kama lilivyoahidi na kusisitiza kuwa, ujenzi wa hospirali hiyo ukamilike kwa wakati na kufikia Oktoba mwaka huu wananchi waanze kupata huduma.



from MPEKUZI

Comments