Mwongozo Wa Udhibiti Wa Ugonjwa Wa Korona (Uviko-19) Kupitia Afua Ya Kuthibiti Misongamano Katika Jamii Bila Kuathiri Shughuli Za Kiuchumi
1. Utangulizi
Kutokana na mwenendo wa ugonjwa wa corona (UVIKO-19) nchini, Kamati ya Wataalamu imeainisha maeneo mahususi yanayohitaji kutiliwa mkazo kupitia afua za kupunguza msongamano katika jamii.
Lengo ni kukata mnyororo wa maambukizi katika ngazi ya kaya na jamii. Mwongozo huu utawawezesha Wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii sambamba na kubadili tabia zao huku wakizingatia mbinu za kujikinga na ugonjwa, kwa kupata elimu ya kutosha, na kujiwekea utaratibu wa kudhibiti ugonjwa kutokusambaa kwenye jamii. Wananchi tayari wamepokea mbinu hizi kwa mtazamo chanya lakini zinahitaji kuimarishwa bila kulega lega ili jamii iweze kujikinga, kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa UVIKO-19.
2. Kusitisha mikusanyiko mikubwa isiyokuwa ya lazima.
Mwongozo huu unasitisha mikusanyiko yote mikubwa ya kijamii, kidini na kisiasa mpaka ugonjwa utakapo dhibitiwa na kutolewa taarifa rasmi na Wizara ya Afya. Pale ambapo patakapohitajika ulazima wa kufanyika shughuli ya Mikusanyiko, kibali kiombwe kuanzia ofisi za serikali za mitaa, kupitia Halmashauri na idhini itolewa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa husika, kwa kuzingatia vigezo vyote vya kinga na usalama wa afya kwa wananchi.
3. Udhibiti wa mikusanyiko katika maeneo mbalimbali.
Maeneo yanayoleta mikusanyiko ni yale ya huduma za Kijamii, Kibiashara, Kiuchumi, Kiofisi n.k ambayo ni mojawapo ya vyanzo vya kusambaa kwa maambukizi katika jamii. Mwongozo huu unalenga kudhibiti ugonjwa huu bila kuathiri shughuli za kiuchumi na maisha ya kawaida ya kijamii ya wananchi. Baadhi ya maeneo hayo ni kama ifuatavyo: -
3.1.1 Vyombo vya Usafiri na Stendi za Mabasi/Daladala/Bodaboda
Ugonjwa wa Corona (UVIKO-19) unaweza kusambazwa kupitia vyombo vya usafiri hivyo hatua zifuatazo hazina budi kuendelea kuchukuliwa;
a) Kuhamasisha na kusimamia kuepuka msongamano na kuzingatia kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu kama kuna uwezekano huo.
i. Wasafiri wawezeshwe kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kabla ya kuingia kwenye vyombo vya usafiri hivyo, viongozi wa mtaa husika wahakikishe kuna vyombo vya kuhifadhia maji na sabuni vya kutosha katika kila kituo. Aidha, uongozi wa vituo vya mabasi usimamie uwepo wa vifaa vya kunawia kwa maji tiririka na kuhakikisha abiria wote wananawa mikono.
ii. Wamiliki wa vyombo vya usafiri wahakikishe wanaweka vipukusi vya kutakasa mikono katika vyombo vya usafiri.
iii. Kila msafiri anayeingia kwenye chombo cha usafiri wa umma lazima awe amevaa barakoa kama ilivyoelekezwa kwenye mwongozo isipokuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 8.
iv. Abiria wote waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutosongamana ndani ya vituo vya Mabasi kupitia walinzi getini, wahudumu wa mabasi na askari wa usalama wa barabarani.
v. Bodaboda wabebe kwa idadi sahihi (1-2) (siyo mishikaki) na wavae barakoa
vi. Stendi zihakikishe zinatoa ujumbe wa kuelimisha jamii ya wasafiri mara kwa mara kupitia vipaza sauti, na wanapokuwa safarini, madereva na wahudumu wa vyombo vya usafiri wahakikishe ujumbe wa kuelimisha unatolewa kwenye chombo mara kwa mara.
vii. Wananchi wakae au kuongozana kwa umbali wa zaidi ya mita moja katika maeneo yote wanayokuwepo kabla ya kuingia kwenye chombo cha usafiri.
viii. Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama; kwa magari maalumu yenye nafasi kubwa kama mwendokasi, inapolazimika kusimama basi kila abairia avae Barakoa na kuachiana angalau umbali wa nusu mita.
b) Upimaji wa dalili za ugonjwa wa Korona (UVIKO-19) na taratibu getini wakati wa kuingia /kutoka ndani ya Mabasi.
i. kupima joto mwili kwa kutumia ‘thermoscanners’ ufanyike getini na kwenye mabasi.
ii. Halmashauri zisimamie maeneo yote ya mabasi yaendayo Mikoani yaanzishe utaratibu wa uchunguzi wa wasafiri, na wale watakaoonesha dalili (ambazo zimeainishwa na Wizara ya Afya) wasiruhusiwe kuendelea na safari badala yake washauriwe kwenda kuonana na wahudumu wa afya.
iii. Magari yote yabandikwe namba ya simu ya dharura (199) itakayosaidia wasafiri wenye dalili za UVIKO-19 kupatiwa msaada muda wowote na mahali popote.
iv. Maafisa wa Usalama Barabarani wafanye ukaguzi wa kushtukiza kuhakikisha uzingatiaji wa maagizo haya ikiwemo utoaji wa jumbe za UVIKO-19.
c) Utaratibu Katika Nyumba za Ibada
Nyumba za ibada zikaguliwe mara kwa mara na kuhakikisha zinazingatia yafuatayo;
i. Ziweke vifaa vya kunawia mikono (maji safi tiririka na sabuni au Vitakasa mikono-Sanitizers) na muumini atakaye simamia unawaji kwa wote.
ii. Waumini wavae Barakoa
iii. Waumini wakae umbali unaozidi mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine pande zote.
iv. Taratibu za kufanya usafi na utakasaji wa viti, meza na maeneo wanapokaa kabla na baada ya ibada ufanyike. Alama katika viti ziwekwe kuonyesha umbali wa mita moja.
v. Wazee, Watoto na wale wote wenye matatizo ya kiafya yanayotambulika (Mfano. Kisukari, Shinikizo la Damu, Kansa n.k), wanashauriwa kujiepusha na ibada zenye mikusanyiko ya Watu wengi na wachukue tahadhari zote muda wote
vi. Kama nyumba ya ibada ni ndogo uanzishwe utaratibu wa kusalia nje/maeneo ya wazi au kuongeza idadi ya vipindi vya ibada na kuruhusu idadi ya watu wachache kuingia ibadani na kuzingatia uvaaji wa Barakoa.
vii. Ibada ziwe za muda mfupi usiozidi masaa mawili.
viii. Huduma zinazohusisha kugusana ziepukwe
ix. Kuwepo na ujumbe wa mara kwa mara kwa ajili ya kuwakumbusha waumini kuhusu namna ya kujikinga na UVIKO-19 na namba za kuwasiliana na huduma za afya iwapo atapatikana mgonjwa.
d. Maeneo ya Baa, Migahawa, Hoteli, Kumbi za Starehe, Mikutano, Harusi na Sherehe mbalimbali
Kimsingi baadhi ya shughuli za kundi hili zinafaa kuangaliwa iwapo ni muhimu? Lazima au zisubiri hali itengamae. Iwapo ni muhimu na lazima mambo yafuatayo hayana budi na ni lazima yazingatiwe;
i. Kuwe na kipima joto kwa wote wanaoingia kupata huduma kwenye eneo husika.
ii. Wamiliki au Waandaaji wa mikutano waweke vifaa vya kunawia mikono maji tiririka na sabuni vinavyotosheleza mahitaji au kutumia vipukusi
iii. Wateja /washiriki wakae umbali wa mita moja kutoka mteja hadi mteja.
iv. Ili kupunguza msongamano usio wa lazima, wateja washauriwe kununua vinywaji na kunywea nyumbani.
v. Sherehe zote za harusi kufanyika nje ya kumbi (open air) au kama zinafanyika ukumbini, ziwe za muda fupi, wageni waalikwa wawe wachache kuruhusu ukaaji wa mita moja au zaidi.
vi. Washiriki wote wa sherehe za harusi/Mikutano wavae barakoa.
vii. Wamiliki wahakikishe wanaweka walinzi na kuhakikisha kila anayeingia kwenye maeneo haya anavaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
viii. Kwenye mikutano ya ofisi za Umma, waraka/barua toka wizara ya utumishi ya 15 Mei, 2020, iendelee kuratibu utendaji wa watuimIshi katika kujikinga na UVIKO-19.
ix. Wamiliki wa Baa/Kumbi za Starehe au Harusi wahakikishe Wahudumu wanavaa Barakoa.
x. Kuwepo na utaratibu katika maeneo haya wa kupunguza watu kuchangamana.
xi. Maeneo haya yakaguliwe na Wataalamu wa Afya na Kamati za Ulinzi na Usalama kuhakikisha maelekezo yanazingatiwa.
a. Maeneo ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya
Vituo vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kutekeleza hatua zifuatazo: -
i. Kuweka bango getini linalohimiza uvaaji wa barakoa na kuepuka misongamano wakati wote wa huduma.
ii. Wagonjwa wa nje wasio na dharura waonwe kwa kupangiwa tarehe maalumu (Appointments) ili kuzuia mlundikano kwa wagonjwa kwa wakati mmoja.
iii. Kwenye maeneo ya kusubiria huduma kwa wagonjwa viwekwe viti vya kutosha na vipangwe kwa kuzingatia umbali wa mita moja au zaidi kila pande ikiwezekana alama ziwekwe kudhibiti msongamano. Penye eneo finyu sehemu za kusubiria ziwekwe hata nje ya jengo la kituo cha kutolea huduma za afya.
iv. Ndugu wa kuona/kuleta mgonjwa wasizidi wawili (2) kwa wakati mmoja na wote watatakiwa kuvaa barakoa na watumie kwa muda usiozidi nusu saa kumuona mgonjwa.
v. Kudhibiti watu wasiohusika kwenye maeneo mbalimbali ya kituo cha afya kutembelea maeneo hayo.
vi. Kuruhusu wagonjwa kwenye kliniki za ufuatiliaji wa kawaida, kuwapigia simu Madaktari Bingwa wakati wa masaa ya kazi hususan kwa wale wanougua magonjwa yasiyohitaji kumwona daktari uso kwa uso ili wapewe ushauri.
vii. Kuwapima joto la mwili watu wote wanaoingia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
viii. Wagonjwa wenye magonjwa sugu wapewe dawa za angalau miezi miwili.
ix. Wagonjwa na wateja wanaohitaji huduma za afya wenye umri wa miaka sitini au zaidi (wazee) wapewe kipaumbele kwenye huduma ili wasichangamane muda mrefu na watu wengine.
x. Vituo vyote vihakikishe vinaweka vifaa madhubuti (Visivyoshikwa kwa mkono-foot/pedal/elbow operated) vyenye maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono (hand sanitizers) katika maeneo yote ya kutolea huduma (every Point of Care).
b. Vituo vya Polisi, Magereza na Mahakama
Vituo vya Polisi vitatakiwa kufanya yafuatayo: -
i. Kuweka maeneo ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni
ii. Watumishi na watu wote wanaoingia katika vituo vya polisi wavae barakoa muda wote.
iii. Kutoa kipaumbele cha dhamana kwa Mahabusu wenye makosa yanayodhaminika kisheria ili kupunguza msongamano.
iv. Kufanya kipimo cha haraka cha UVIKO -19 kwa mahabusu wote wanaofikishwa gerezani kwa mara ya kwanza.
v. Kuwapima joto la mwili watu wote kabla ya kuingia kituoni na chumba cha Mahabusu.
vi. Kuruhusu ndugu mmoja tu kumtembelea mfungwa, kumuona mahabusu katika siku iliyotengwa na kuhakikisha wafungwa na ndugu wote wanavaa barakoa na wanakuwa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.
vii. Wasikilizaji wa kesi mahakamani wazingatie kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu
c. Saluni pamoja na Vinyozi.
Maeneo ya Saluni na vinyozi ni lazima yakaguliwe mara kwa mara na maafisa afya wa Halmashauri na kuhakikisha mambo yafuatayo yanazingatiwa; -
i. Wamiliki wa Saluni na Vinyozi wanatakiwa kuwa na vifaa vya kutosha vya kuwezesha unawaji wa mikono nje ya saluni ambapo kila atakayeingia katika eneo hilo atahitajika kunawa mikono au kutakatisha mikono kwa kutumia vitakasa mikono vyenye kiwango cha alcohol asilimia isiyopungua 70%.
ii. Kuhakikisha upimaji wa joto la mwili kwa wateja kabla ya kuingia saluni na kwa vinyozi pale inapowezekana.
iii. Kuhakikisha uwepo wa taulo zilizofuliwa, kukauka na kupasiwa za kutosha kulingana na wingi wa wateja. Kila mteja atumie taulo lake lililo safi. Pale ambapo wateja huvishwa joho la kufunika mwili, mhudumu ahakikishe mteja amezungushiwa tissue shingoni kabla ya kumvika joho hilo. ‘Tissue’ isitumike zaidi ya mara moja.
iv. Kuhakikisha hakuna msongamano wa watu na kwamba kila kiti kiwe katika umbali wa mita moja na kuendelea na pale inaposhindikana wateja wasubiri nje.
v. Utakasaji wa vifaa vinavyotumika katika maeneo hayo ufanyike kila wanapomhudumia mteja kwa kutumia vitakasa vyenye alcohol asilimia 70 kama spirit.
vi. Kuhakikisha Saluni zinakuwa safi wakati wote.
vii. Kuhakikisha uvaaji wa barakoa muda wote kwa watoa huduma na wateja.
viii. Barakoa hizi ziwe zinatumika mara moja kila baada ya masaa 4 na ivaliwe barabara kuhakikisha inafunika mdomo na pua.
ix. Kuhakikisha wateja wenye joto kali la mwili, mafua na kikohozi hawaingii saluni (Weka Tangazo), waelekezwe kwenda kupata matibabu kwenye vituo vya afya.
x. Endapo Saluni/Vinyozi wanahuduma ya massage au kuosha, watoa huduma wahakikishe uvaaji wa gloves pamoja na barakoa muda wote wanapotoa huduma.
xi. Kusimamia utaratibu wa kunawa mikono kwa kila mteja anayeingia.
xii. Weka chombo cha kuhifadhia taka na hakikisha taka za barakoa na tissue zinachomwa.
d. Masoko, Magulio, Minada, Maduka makubwa na Maeneo mengine ya biashara
Mambo yafuatayo yanahitaji kuzingatiwa;
i. Halmashauri ziandae timu za kukagua maeneo haya inayojumuisha viongozi wa ngazi za jamii ili kupunguza misongamano katika maeneo husika.
ii. Halmashauri iainishe maeneo zaidi na kuangalia namna ya kupunguza msongamano ikiwa ni pamoja na kutumia viwanja vya mipira wa miguu au maeneo yoyote yaliyo wazi kwa ajili ya huduma za masoko au kushushia bidhaa. Lengo ni kuwawezesha wafanyabiashara na wateja kuwa kwenye umbali unaokubalika na kuweka utaratibu kwa wateja kukaa umbali wa mita moja au zaidi wakati wa kupata huduma
iii. Kuweka utaratibu kwenye maeneo ya kuingilia ili kuhakikisha kila mteja na mfanyabiashara anayeingia kupata huduma katika maeneo hayo awe amevaa barakoa au aelekezwe kununua barakoa bila shuruti
iv. Kila mwenye biashara aweke chombo chenye maji tiririka na sabuni na kila mara awaelekeze wateja wake kunawa kabla hawajaingia sokoni au dukani kupata huduma.
v. Watu wasiokuwa na kazi maalumu wasiruhusiwe kukaa katika maeneo hayo ili kupugunguza msongamano.
vi. Watu waelimishwe ikiwezekana wanunue mahitaji ya kuwawezesha kukaa muda mrefu ili kupunguza uwezekano wa kwenda kwenye maeneo hayo mara kwa mara
vii. Minada iepuke shughuli zinazofanya watu kukaa muda mrefu na kuchangamana zaidi kama uchomaji wa nyama (watu wanunue na kupeleka nyumbani) au unywaji wa pombe.
viii. Kuweka au kutumia vipaza sauti kwa ajili ya kuhimiza kanuni za afya na matangazo mbalimbali.
ix. Kuwashauri wazee, watoto na watu wenye magonjwa ya muda mrefu kuepuka kwenda kwenye mikusanyiko ikiwezekana wawaombe vijana kuwasaidia kuwanunulia mahitaji.
x. Iwapo kwenye maeneo haya kuna biashara mbalimbali zilizotajwa awali, utaratibu wake uzingatiwe kama ilivyokushaelezwa mfano Baa, Kumbi za Harusi, Saluni nk
e. Shughuli za Michezo na Matamasha ya Muziki
Mazoezi na shughuli zote za michezo ni sehemu muhimu katika kuimarisha afya na kujikinga na magonjwa mbalimbali. Hata hivyo shughuli hizi zinatakiwa kufuata mwongozo wa kuzingatiwa kuendesha shughuli za michezo katika kipindi cha Mlipuko wa covid 19 nchi kwa lengo la kudhibiti maambukizi ambao uliytolewa na Wizara ya Afya Mei 2020. Hata hivyo kwa matamasha ya muziki, burudani na sanaa nyingine na ambayo yameidhinishwa na BASATA waandaaaji watahakikisha kuwa matamasha hayo yanafanyika zaidi kwenye maeneo ya wazi (viwanjani), ambapo kabla ya kuingia uwanjani waandaaji watahakikisha kuwa washiriki wananawa mikono kwa maji tiririka/kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa uwanjani. Kamati za ulinzi na usalama za Mikoa katika kuridhia matamasha haya, zitajiridhisha kwanza na uzingatiaji wa masharti haya. Aidha, kwa shughuli zote za sanaa zinazolazimika kufanyika ndani ya kumbi waandaaji watahakikisha zitazingatia Kanuni zote hizi na ile ya kuhakikisha watu wanakaa umbali wa mita moja.
Kuimarisha na kuongeza mbinu za utoaji wa elimu ya UVIKO-19 kwenye Mikusanyiko
Utoaji wa elimu ya afya kwa umma utaendelezwa kila siku kwa kuhusisha mbinu mbalimbali na wadau mbalimbali kwa kufanya yafuatayo;
i. Kuendelea kutumia vyombo mbalimbali vya habari katika utoaji wa elimu ya afya kwa umma.
ii. Kuhamasisha wananchi kuhusu tahadhari na namna ya kuendeleza jitihada za kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuhusisha makundi mbalimbali ya kijamii.
iii. Kutumia magari ya matangazo (PA system) na vipaza sauti (megaphones) katika kufikisha jumbe mbalimbali kwa jamii
iv. Kutumia vikundi vya Jamii/Jadi, Sanaa kufikisha jumbe na pia kutumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) na pia kutumia wataalam wa maendeleo na ustawii wa jamii katika kutoa elimu ya afya kwa jamii kwa kutembelea kaya pamoja na kuwafuatilia watu wanaohisiwa au kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa aijili ya kuwapa elimu ya kupata huduma na kuwakinga wengine wasipate ugonjwa.
v. Kutumia lugha ya Alama na maandishi ya nukta nundu kwa watu wenye ulemavu iliwawezekupata elimu stahiki
vi. Katika kupokezana Microphone, tahadhari zichukuliwe za kutumia vipukusi pale inapolazimu watumiaji zaidi ya mmoja
Matumizi ya Barakoa katika Misongamano
Matumizi ya Barakoa kwa wananchi wote kwenye sehemu zenye mikusanyiko (Mass Masking) ni hatua muhimu ya kukata mnyororo wa maambukizi katika jamii. Aidha, matokeo ni makubwa sana pale ambapo uvaaji barakoa unaenda sambamba na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na au kutumia vitakasa mikono. Pamoja na jitihada za kudhibiti misongamo kufanyika ni vyema pia wananchi waendelee kuhamasishwa kuvaa barakoa wanapotoka majumbani kwao pamoja na wale wote wenye dalili. Ni muhimu kwa mtu yoyote ambaye hataweza kuwa mbali na mtu mwingine kwa zaidi ya mita moja, ahakikishe anavaa barakoa muda wote anapokuwa na mtu ambaye hakai naye nyumba moja. Uvaaji wa barakoa utasaidia kupunguza maambukizi mengine ya mfumo wa hewa;
Hivyo tunapendekeza kuwa; -
i. Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Kata, Vijiji na Mitaa, ihakikishe wananchi wanaelimishwa namna sahihi ya kuvaa, kuvua, kufua, kupasi na kutunza barakoa.
ii. Mamlaka za Wilaya/Halmashauri Kata na Serikali za Mitaa zihakikishe zinaelimisha na kufanya ufuatiliaji zaidi wa uvaaji wa barakoa za aina zote katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko kama ifuatavyo:
iii. Kwenye daladala, mabasi na magari mengine ya abiria, lazima kila dereva na kila abiria avae barakoa;
iv. Kwenye maeneo yote ya mikusanyiko kama sokoni, dukani, stendi, saluni, hospitali, viwanja vya ndege, kwenye meli/mtumbwi, gengeni, kanisani, mashuleni/vyuoni, mabaa, harusi, sherehe au mikutanoni, kila mmoja avae barakoa.
v. Elimu itolewe ya kutosha kuhusiana na utengenezaji, matumizi sahihi na utupatikanaji wa Barakoa.
vi. Elimu juu uandaaji, uuzaji, Uvaaji na utumiaji sahihi wa Barakoa utolewe kwa umma kuanzia ngazi ya Kaya na Mitaa.
Mwisho, Wakuu wa Mikoa. Wilaya na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viwasaidie Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika kutekeleza Sheria ya Afya ya Jamii (Public Health Act 2009) kipengele cha 15 na 16 inayawapa mamlaka ya kuthibiti kusambaa kwa magonjwa katika maeneo yao kwa kusimamia mbinu mbalimbali za uthibiti kwa jinsi watakavyoshauri.
Imetolewa na.
Prof.Dr. Abel N. Makubi
KATIBU MKUU
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
25 July 2021, Dar es Salaam
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment