Mbowe Afikishwa Mahakamani na Kusomewa Makosa ya Ugaidi


Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana  na kusomewa mashtaka mawili ikiwemo la ugaidi.

Mbowe amefikishwa katika Mahakama hiyo jana  July 26, 2021 na kusomewa mashataka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Tulimanjwa Majigo amesema kuwa Mbowe anaunganishwa na Washtakiwa wengine watatu waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka mengine yote ya ugaidi wanayodaiwa kuyatenda mwaka 2020.

Katika kosa la kwanza Mbowe anadaiwa kula njama ya kutenda kosa ambapo anadaiwa kula njama hiyo kati ya Mei na Agosti 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro, kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi kati ya tarehe hizo tajwa.

Baada ya kusomewa maelezo Mbowe hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka, kesi imeahirishwa hadi Agosti 5, 2021 na upelelezi umekamilika ambapo zinasubiriwa nyaraka ili ihamishiwe Mahakama kuu.



from MPEKUZI

Comments