WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haijamlazimisha na wala haitamlazimisha mwananchi kuchanjwa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19, hivyo amewataka Watanzania wapuuze upotoshaji unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
"Hakuna aliyelazimishwa kuchanja chanjo hiyo na wala hakuna mahali palipoandikwa kwamba lazima wananchi wachanjwe. Chanjo ni hiari tusipotoshane kwa sababu hakuna Serikali inayoweza kuandaa mpango wa kuwaangamiza wananchi wake."
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 27, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nandagala ambapo amewasisitiza waendelee kuchukua tahadhari na kujikinga na UVIKO 19.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeleta chanjo hiyo ili kutoa fursa kwa Watanzania watakaohitaji kuchanjwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 waweze kuipata kwa ukaribu na urahisi zaidi na si vinginevyo.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza Watanzania waendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka na sabuni, watumie vitakasa mikono pamoja na kuvaa barakoa zilizothibitishwa na mamlaka husika.
Mbali na maelekezo hayo, Pia Waziri Mkuu amesema ni vema kwa sasa wananchi wakajiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na inapolazimu basi wazingatie kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka mtu mmoja hadi mwingine lengo likiwa ni kujikinga na UVIKO 19.
Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi wanatakiwa wafanye mazoezi ya mara kwa mara kulingana na afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka, pia amewasihi wazingatie lishe bora.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwamba Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya yao na Tanzania kwa ujumla, hivyo waendelee kuiamini Serikali yao.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi. Amewataka waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.
Amesema tatizo la maji wilayani Ruangwa linaenda kuwa historia kwa sababu Serikali inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ambao unatoa maji Ndanda hadi Ruangwa. “Mradi huu mkubwa utapunguza tatizo la upatikanaji wa maji wilayani Ruangwa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba atasimamia ipasavyo kuhakikisha mradi wa maji wa Mbwinji-Ruangwa unakamilika kwa wakati ili wananchi wa wilaya hiyo waweze kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.
Aweso amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote nchini, amewaomba wananchi waendelee kuwa na subra.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment