Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya usambazaji wa chanjo za UVIKO-19 katika mikoa yote hapa nchini.
Ugawaji wa chanjo umezingatia taarifa ya visa vya wagonjwa waliohisiwa kuwa na UVIKO-19, idadi ya walengwa kwa kundi la kipaumbele pamoja na idadi ya chanjo zilizopatikana kwa sasa. Aidha, Serikali kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa na Vyombo vingine, vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa hizi chanjo za Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani.
==>>BONYEZA HAPA KUJUA VITUO VITAKAVYOTOA CHANJO YA CORONA TANZANIA
Kutokana na Mwongozo wa Chanjo wa Taifa dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO, ule Shirika la Afya Duniani (WHO), maelekezo ya COVAX FACILITY na upungufu wa uzalishaji wa chanjo toka viwandani, Chanjo hizi KWA SASA zinatolewa kwa kufuata vipaumbele vya makundi yenye uhitaji mkubwa ambayo ni (1) Watumishi wa sekta ya Afya, (2) watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na (3) watu wenye magonjwa.
Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza, uchanjaji kwa makundi yote nchini ni wa hiari au huru kwa kila mwananchi. Kwa kuwa chanjo zilizopokelewa kwa sasa hazitoshelezi walengwa wa makundi yote nchini, makundi mengine yatapata chanjo katika awamu inayofuata, mara zitakapowasili.
Serikali inategemea kutoa chanjo kwa makundi yanayolengwa kuanzia tarehe 3 Agosti 2021, siku ya Jumanne, katika vituo 550 vya kutolea huduma katika mikoa yote ya Tanzania bara. Orodha ya vituo hivyo inapatikana pia katika tovuti ya wizara;
www.moh.go.tz.
Wananchi wote walengwa, wanaotaka kuchanjwa kwa hiari yao, wanatakiwa kufanya mambo yatuatayo;
1. Kujihakiki kama wapo ndani ya makundi matatu (3) ya walengwa kwa sasa.
2. Kuandaa kitambulisho cha Kazi, NIDA, Leseni ya Udereva, Mpiga kura,
Pasi ya Kusafiria au kitambulisho chochote kinachotambulika kisheria.
3. Kufanya “booking” ya siku ya kuchanjwa kwa kutumia mtandao ndani ya simu /Computer (online) yako kupitia https://ift.tt/2WE1Xcv au kwa kwenda moja kwa moja kwenye kituo na kujisajili kuanzia Jumatatu tarehe 2 Agosti
2021
4. Kujaza fomu ya uhiari wa kuchanjwa,
Wizara inaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini, kukamilisha matayarisho yote muhimu kwa utoaji wa chanjo, ili ifikapo tarehe 03 Agosti 2021, utoaji wa chanjo uwe umeanza katika vituo vilivyoainishwa katika mikoa.
Kutokana na uhitaji na mipangilio ya Mkoa husika, wanaweza kuongeza idadi ya vituo ili kupunguza msongamano katika vituo.
Aidha, katika zoezi hili, wananchi, watasajiliwa katika mfumo wetu wa Taifa wa Chanjo na watapatiwa cheti baada ya kuchanjwa.
Naelekeza pia kwa huu mgao wa COVAX FACILITY ni marufuku Hospitali yoyote (ya umma au binafsi) kulipisha Wananchi gharama yoyote katika zoezi hili la chanjo na lifanyike kwa uadilifu na kwa haki kwa walengwa wa sasa.
Pamoja na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufanikisha upatikanaji wa chanjo nchini na kuanza kuchanja Wananchi, Wizara ya afya inaendelea kuwashauri Wananchi kuendelea kujikinga na UVIKO-19 kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali za mita moja au zaidi, kuepuka misongamano na kufanya mazoezi.
Mwisho, napenda kurudia tena kuishukuru Serikali yetu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya Marekani, kwa kufanikisha upatikanaji wa chanjo hizi ambazo zimepitia kwenye mpango huo wa COVAX. Pia nawashukuru wadau wetu wote wa chanjo kwa michango yenu mikubwa katika kufanikisha upatikanaji wa chanjo.
Aidha Serikali inawapongeza sana Viongozi wetu na Wananchi ambao tayari wameitikia zoezi la kuchajwa kwa hiari.
Imetolewa na
Prof. Abel N. Makubi
KATIBU MKUU (AFYA)
Dar es Salaam, 30 Julai 2021
==>>BONYEZA HAPA KUJUA VITUO VITAKAVYOTOA CHANJO YA CORONA TANZANIA
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment