Taaluma Ya Famasi Ni Muhimu Katika Vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza- Dr. Gwajima


Na. Catherine Sungura,WAMJW-Mwanza
Katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza Taaluma ya Famasi ni muhimu katika kuwezesha upatikananji wa bidhaa  za dawa  kwa wale watakaoshindwa  kuzuia kupata  magonjwa yasiayoambukiza na ikawalazimu wafike vituoni  kupata tiba.


Kauli hiyo imetolewa jana  na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Kongamano la 12 la kisayansi la Chama cha Wanafunzi wa Taaluma ya Famasi (TAPSA) lililofanyika jijini Mwanza.


Dkt. Gwajima amebainisha kwamba bidhaa hizo za dawa kwa ajili ya kundi hilo  ni ghali na bahati mbaya  nchini Tanzania hakuna  kiwanda cha kutengeneza  na badala  yake wanaagiza toka nje ya nchi.“Tunapaswa kutafakari iwapo kasi ya kukua kwa maradhi haya ni inaongezeka je tunazijazititi vipi kwenye kasi ya kinga kwani bado kasi hiyo ni ndogo”.Aliongeza Dkt. Gwajima.


Alisema kuwa, katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza Serikali  imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora  karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu , kuajiri watumishi na kuweka vifaa tiba  na dawa. Maboresho haya yameendelea kufanyika katika vituo vya huduma  za afya ngazi zote.


Hata hivyo amesema  kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo changamoto ya upatikanaji  wa bidhaa  za dawa  na vifaa tiba kwa ajili  ya huduma mbalimbali zikiwemo  na huduma kwa ajili ya wanaougua magonjwa hayo yasiyoambukizwa.


Aidha, Dkt. Gwajima amesema wapo baadhi ya wanataaluma wachache  wasio waadilifu na wasio wazalendo ambao ni doa kubwa kwenye  taaluma hiyo adimu ambayo inatarajiwa kuwa  na mchango mkubwa  kwenye ajenda ya afya. Hivyo  iwapo itasimama kwa nafasi yake basi  wanataaluma  hao wanaweza  kufanya mapinduzi  makubwa  ya afya na kiuchumi.


“hii itawezekana kwa kujikita  kwenye ajenda  ya jinsi gani  viwanda vya ndani  viweze kuzalisha  bidhaa mbalimbali  na kuhakikisha  matumizi yasiyotia shaka  ya bidhaa za afya  zinazopokelewa kwenye  vituo vya huduma  na kuepuka upotevu na matumizi yasiyofuata  miongozo na kusababisha usugu wa baadhi ya dawa na pia  baadhi kuleta madhara kwa wateja  kama ilivyokusudiwa”.


Dkt. Gwajima alitoa rai  kwa jamii  ya kitanzania kuzingatia ulaji unaofaa   ambapo kila mlo uwe na  makundi yote matano  ya vyakula  halisi, kutotumia  mafuta mengi,chumvi nyingi,kufanya mazoezi ,kupata usingizi wa kutosha,kuepuka matumizi ya tumbaku na madawa ya kulevya  na pia kuchunguza afya angalau mara moja kwa mwaka.


Takwimu zinaonyesha  kuwa asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinavyohusu watu  wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa hayo.Hapa nchini  inakadiriwa kuwa magonjwa yasiyoambikiza  husababisha asilimia 27 ya  vifo  vyote.Kauli mbiu ya Kongamano hilo mwaka huu  ni “Wataalamu wa Famasi: kuongeza wigo katika kupambana  na magonjwa yasiyoambukiza”. 


Awali akiongea wakati wa kongamano hilo Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi aliwataka wafamasia na wataalum wengine wa afya nchini kuhakikisha wanatumia fomu za dawa( prescription form) kama nyenzo muhimu za kuondoa changamoto za dawa kwani dawa ni fedha za haraka hivyo wahakikishe kabla hawajatoka lazima wahakikishe dawa zinatoka kwa kujaza fomu hizo.


Aliongeza kuwa kwenye kutenda kazi za umma lazima wafuate miongozo ikiwemo muongozo wa matibabu  nchini (STG) wanapokuwa sehemu za kazi hivyo ni wakati wao sasa wa kupitia na kuelewa nini wanapaswa kutekeleza kwenye kazi zao.


Hata hivyo Bw. Msasi aliwataka chama hicho kuanziasha klabu za mazoezi kwenye vyuo vyao ili kuweza kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa vitendo na hiyo itasaidia jamii kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi.


Naye Mlezi wa wanafunzi wa Famasi na Masajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth shekalaghe aliwataka wanafunzi hao kufanya kazi kwa kujitoa, kuwajibika na kuipenda taaluma  yao ili kuweza kuitumikia vyema taaluma yao.


Bi. Shekalaghe alisema kama Baraza wataendelea kusimamia na kuhakikisha wanaendeleza taaluma  kwa kutoa elimu ya maadili kwenye vyuo vya famasi nchini ili wanapokua chuoni wazitambua na kuzijua angali wanafunzi.


Naye Rais wa Chama cha Wafamasia Wanafunzi Tanzania(TAPSA) Bw. Hamis Msagama ameipongeza Serikali kwa uboreshaji wa dawa na vifaa tiba ambapo kazi kubwa inafanywa na wafamasia  na kuonesha jinsi gani  inawajali watanzania.


Pia Bw.Msagama ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuanzisha kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD)  hivyo wao kama chama waliona ni vyema kongamaono lao  mwaka huu kujadili kwa kina namna ya kupambana na magonjwa hayo ambayo yanaathiri watu wengi nchini na duniani.



from MPEKUZI

Comments