Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma
Serikali inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wa Umma wakiwemo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kufanyakazi kwa weledi na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa Umma wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimali watu Bi. Zahara Guga katika kikao na watumishi kilichofanyika Makao Makuu wa Wizara hiyo yaliyopo Mji wa Magufuli Mtumba Jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi hao ikiwa na sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa umma kwa mwaka 2021.
“Viongozi wetu wapo pamoja nasi wanatambua mchango wenu katika kulitumikia taifa, hii ni wiki ya kutoa huduma kwa wananchi na sisi tunaofanyakazi tujitahidi kutoa huduma iliyoyukuka kwa wadau wetu na wananchi” amesema Bi. Guga.
Bi. Guga ameongeza kuwa lengo la Wiki ya Utumishi wa Umma ni kutambua mchango na umuhimu wa Watumishi wa Umma katika kuleta maendeleo katika taifa ili kutoa motisha na ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
Malengo mengine ni kuwezesha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia dira, dhima, malengo, programu na mikakati kwa lengo la kutoa huduma kwa umma, kuhamasisha na kuwapa motisha Watumishi wa Umma waendelee na kazi ya ujenzi wa Taifa na kuwa wabunifu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Aidha, Siku ya Utumishi wa Umma inasaidia Serikali kupata mrejesho kutoka kwa wateja/wananchi na wadau wanaohudumiwa ili kurekebisha kasoro za utendaji zinazosababisha malalamiko ya wateja dhidi ya huduma zinazotolewa na taasisi za umma.
Katika kikao hicho, Bi. Guga amemtaja Ombeni Andrew kutoka Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuwa ndiye mtumishi hodari kwa mwaka 2021 na watumishi bora kutoka Idara na Vitengo vya mbalimbali ambao ni Ernest James kutoka Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Francis Songoro kutoka Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Sephania Motela kutoka Idara ya Maendeleo ya Utamaduni.
Watumishi wengine ni Yona Haji kutoka Idara ya Habari, Gervas Mbilinyi kutoka Idara ya Sera na Mipango, Rosemary Maganda kutoka Idara ya Maendeleo ya Michezo, Sudi Juma kutoka Kitengo cha Uhasibu na Fedha, Zainabu Omary kutoka Kitengo cha Ukaguzi wa ndani, Keneth Mkumbo kutoka Idara ya Ununuzi na Ugavi, Shamimu Nyaki kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Amina Nguli kutoka Kitengo cha Sheria pamoja na Joakimu Mganga kutoka Chuo cha Mendeleo ya Michezo Malya.
Hii ni siku maalumu ya watumishi wa umma ambayo husherehekewa Juni 23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo chimbuko lake ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers nchini Morocco mwaka 1994.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment