Na Munir Shemweta, WANMM MBEYA
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza zoezi la kutambua vipande 17,000 vya ardhi katika kata sita zenye mitaa 32 katika halmashauri ya jiji la Mbeya.
Hatua hiyo ni jitihada za Wizara ya Ardhi kuhakikisha inatambua maeneo yote yaliyojengwa kiholela nchini ambapo katika kata hizo Wizara imetoa jumla ya Shilingi milioni 145 kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Sinde katika halmashauri ya jiji la Mbeya mwishoni mwa wiki Mratibu wa zoezi hilo ambaye ni Mpima wa mkoa wa Mbeya Leosi Mwenda alisema kuwa kwa sasa zoezi hilo limeanza kwenye kata mbili za Sinde na Ilemi zenye jumla ya mitaa kumi na mbili.
‘’Hivi sasa vijana wapo kazini katika Kata mbili kwa ajili ya utambuzi wa vipande vya ardhi na katika zoezi hilo vijana wanatumia simu janja katika kufanikisha zoezi hilo na mfumo wenyewe wa utambuzi utasomeka Wizarani’’ alisema Mwenda.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo, kabla ya kuanza zoezi hilo timu yake ilikutana na viongozi wa maeneo yanayopitiwa na zoezi hilo wakiwemo madiwani, watendaji na wenyeviti wa mitaa pamoja na mabalozi kuwapatia semina elekezi kwa nia ya kuwajengea ufahamu wa zoezi hilo.
Mwenda alisema, Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa linakofanyika zoezi wamefanya kazi kubwa ya kuwafahamisha wananchi kuhusiana na zoezi hilo na kuwafanya kulipokea vizuri na hivyo kufanya kazi kuwa nyepesi.
Alizititaja kata zitakazofikiwa na zoezi hilo la utambuzi katika halmashauri ya jiji la Mbeya kuwa ni kata za Ilemi, Isanga, Sinde, Meanga, Mabatini pamoja na Nzovu ambazo zote kwa pamoja zina jumla ya mitaa 32.
Kwa upande wake Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Advent Tweve alisema kazi kubwa ya zoezi hilo ni kufanya utambuzi wa vipande vya ardhi katika makazi holela na kuwapatia wamiliki wake leseni za Makazi ambapo alieleza kuwa, kabla ya kuanza zoezi hilo kuliundwa kamati za wananchi kwenye mitaa kwa lengo la kutatua changamoto na kutoa taarifa sahihi kwa wamiliki katika mitaa husika.
Kwa mujibu wa Tweve, leseni za makazi zitakazotolewa ni nyaraka kama zilivyo nyaraka nyingine za ardhi ingawa hizo hutolewa katika maeneo yasiyopangwa na kupimwa na gharama yake ni ndogo ukilinganisha na ile ya hati.
Naye Diwani wa Kata ya Sinde Fanuel Kyanula aliwaeleza wananchi wa kata yake kuwa zoezi la utambuzi kila kipande cha ardhi linatoa uhakika wa wamiliki na kubainisha kuwa wananchi hao mara kadhaa walishindwa kuendeleza vibanda vyao kwa hofu ya kubomolewa maeneo yao.
‘’Sasa hivi zoezi hili la utambuzi linawataka mtoe 10,000 tu , ningependa jambo hili liende haraka katika kata hii ya Sinde na ii inaonesha serikali imesikia kilio cha wananchi wengi na tuchangamkie haraka sana na muwe na amani’’ alisema Kyanula.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment