Na Happiness Shayo – TUNDURU
Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza operesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia na kufanya shughuli zao katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere na maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya utalii na uhifadhi wa wanyama mkoani Ruvuma.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akiongea na wananchi wa vijiji vya Kalulu na Jakika wilayani Tunduru, wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero ya wananchi kuhusiana na wanyamapori wanaovamia mashamba na kufanya uharibifu wa mazao wilayani humo.
Alisema, tatizo la wanyama hususani Tembo wanaokula mazao ya wakulima limechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye maeneo yasioruhusiwa kisheria jambo linalosababisha wanyama hao kukimbia.
Kwa mujibu wa Dkt. Ndumbaro Serikali imeshatenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za ufugaji, lakini kutokana na kiburi cha fedha wafugaji wanawatumia baadhi ya wenyeviti na watendaji wa serikali za vijiji wasiokuwa waaminifu kukaidi kupeleka mifugo kwenye maeneo waliyotengewa.
Dkt Ndumbaro amewaonya wenyeviti na watendaji hao kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kupokea fedha na kuruhusu wafugaji kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya utalii kwani tabia hiyo ni kukiuka sheria za utumishi wa umma.
Waziri Ndumbaro, amewataka wananchi kuepuka kuishi na kufanya shughuli zao kwenye hifadhi kwani serikali haitahusika kulipa fidia wala kifuta machozi kwa mtu atakayepoteza maisha, kujeruhiwa na kuharibiwa mazao.
Aidha alisema, ili kukabiliana na wanyama wanaovamia mashamba na kuharibu mazao, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kutoa mafunzo kwa vijana kwenye vijiji vinavyozungukwa na hifadhi na mapori ya akiba ili kuwajengea uwezo wa kufukuza wanyama pindi wanapofika kwenye makazi ya watu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alisema, wilaya hiyo ni ya kilimo lakini changamoto kubwa kuvamiwa na wafugaji na mifugo mingi kutoka katika maeneo mengine ya nchi jambo lililosababisha kutokea kwa migogoro kati ya jamii ya wafugaji na wakulima.
Alisema, licha ya serikali ya wilaya kutenga zaidi ya vitalu 200 vya ufugaji, lakini jambo la kusikitisha baadhi ya viongozi wa ngazi za vijiji wanaruhusu wafugaji kupeleka mifugo kwenye maeneo yasioruhusiwa.
Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alisema, katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali ya wilaya inafanya operesheni za mara kwa mara kuwaondoa wavamizi wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi na maeneo yote yasiyoruhusiwa.
Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo, wameiomba serikali kupitia upya viwango vya fedha vinavyotolewa kwa waathirika wa matukio ya kushambuliwa na wanyama wakali na wanaoharibu mazao kwani havilingani na hasara inayotokea.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Tunduru, Ajili Kalolo alisema, wananchi wanalazimika kuondoa mazao yao mashambani kabla hayajakomaa ili kuepuka kuliwa na wanyama.
Kalolo alisema, kama serikali itaendelea na msimamo wake wa kuwaona wananchi ndiyo wenye makosa kwa kile kinachodaiwa kuvamia kwenye hifadhi basi kuna hatari wilaya hiyo kukumbwa na janga la njaa.
Msanga Rashid mkazi wa kijiji cha Kalulu, ameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuwasaidia kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu wa mazao, badala ya kuwaona wananchi ndiyo wakosaji kwani kama serikali itaendelea na msimamo huo kuna hatari baadhi ya vijiji kutokuwa na watu kwa kuuawa na wanyama.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment