Raia 29 wa Burundi kortini wakidaiwa kuingia Nchini Tanzania bila kibali


Raia 29 wa Burundi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuingia nchini Tanzania bila kuwa na kibali.

Baadhi ya washtakiwa  hao ni Kasimu Kesi, Elias Shadra, Hilary Lozo, Richard Dismas, Ntahondereye Reverie, Nataka Yosam, Meraki Noah, Robert Lazaro, Samson Erick, Kazimana Aimable, John Ayoub na wengine 18.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao janaJumatano Mei 26, 2021 na wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Ngwijo alidai Mei 25, 2021 katika eneo la Kariakoo, washtakiwa hao walikamatwa baada ya kudaiwa kuingia  nchini kinyume cha sheria.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalowakabili, Hakimu Shaidi aliwauliza kama tuhuma zinazowakabili zina ukweli wowote.

Washtakiwa 16 kati ya 29 walikiri makosa huku wenzao 13 wakikana.
 
Wakili wa Serikali, Godfrey, aliomba mahakama iahirishe kesi ili ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Shaidi alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa waliokiri na kuwapa muda washtakiwa waliokana, kutafakari na kufika na vibali vilivyowaruhusu kuishi nchini.

Kesi itakuja Juni Mosi mwaka huu na washtakiwa wote walipelekwa mahabusu isipokuwa watoto ambao walikabidhiwa kwa Idara ya Ustawi wa Jamii hadi tarehe ya kesi ijayo.



from MPEKUZI

Comments