Wafanyakazi Wa Wma Watakiwa Kufanya Kazi Kwa Weledi, Ubunifu, Na Bidii Huku Wakiaswa Kuachana Na Vitendo Vya Rushwa Na Ukandamizaji
Na Eliud Rwechungura
Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) wametakiwa kufanya kazi kwa Weledi, ubunifu na bidii kubwa ili waweze kuwafikia walengwa wengi kwa kukagua vipimo vingi zaidi huku wakiaswa kuachana na vitendo vya rushwa, ukandamizaji wa wateja ili kuondokana na hali ya kupoteza mapato ya Serikali.
Ameyasema hayo, Mwenyekiti wa bodi ya Wakala wa Vipimo Tanzanai, Eng.Dkt, Adelhelm Meru, leo Aprili 23, 2021 Misugusugu, Mkoani Pwani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara wa Viwanda na Biashara, Dotto James wakati wa mkutano wa 29 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo Tanzania wenye lengo la kujadili Mpango na Bajeti katika Kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22.
‘‘Nawahimiza Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa WMA waendelee kufanya kazi kwa weledi na bidii kubwa kusudi tuweze kuwafikia walengwa wengi zaidi kwa kukagua vipimo vingi zaidi lakini pia kuongeza ukusanyaji wa maduhuri kutoka bilioni 27 za sasa na kufikia zaidi ya Bilioni 30 ’’ amesema Mwenyekiti wa bodi ya Wakala wa Vipimo Tanzanai, Eng.Dkt, Adelhelm Meru.
Aidha, Eng.Dkt, Adelhelm Meru ameeleza kuwa kupitia kikao cha wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Wakala wa Vipimo Tanzania watapitia bajeti ya Wakala kwa mwaka wa fedha 2021/22 ikiwa ni utamaduni uliozoeleka ili uongozi uweze kuendana na wafanyakazi wake ni vizuri kuwashirikisha wafanyakazi.
‘’Tunajua kwamba ili uongozi uweze kuendana na wafanyakazi ni vizuri kuwashirikisha wafanyakazi katika masuala haya ya bajeti kwani ni hatua moja inaonyesha wakala wa vipimo haiwaachi mbali wafanyakazi wake kushirikiana nao katika mambo yote yanayohusu hatima ya wakala wanayoongoza,’’alisema Eng.Dk, Adelhelm Meru
Eng.Dkt, Adelhelm Meru amewasisitiza wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo Tanzania kuondokana na hali ua kufanya kazi kwa mazoea huku akiwataka kufanya kazi kwa tija, weledi na ubunifu huku akiwasii kuwa waadilifu na kuacha na vitendo vya rushwa kwa sababu rushwa inaharibu sifa ya mfanyakazi pia rushwa inawakandamiza walaji ambao wanapaswa kuwalinda huku ikisababisha kupoteza mapato ya serikali
Kwa Upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Tanzania, Stella Kahwa ameeleza kuwa lengo kuu la kikao hicho cha baraza ni kujadili bajeti ya WMA ambapo mpaka sasa wakala ya vipimo ina mikoa 29 na bajeti yao inaanza kutengenezwa kuanzia ngazi ya mkoa
‘‘Bajeti lazima iwe shirikishi na ikiwa shirikishi ni rahisi kutekelezeka, hiki tunachojadili ni majumuisho ya bajeti ndogondogo zilizotengenezwa kuanzia ngazi ya mkoa,’’amesema Kaimu Ofisa Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Tanzania, Stella Kahwa.
Stella Kahwa ameendelea kueleza kuwa kikao hicho wamekuja kuelekezana ili mikoa iweze kujuana bajeti zao ili wajue mkoa huu una bajeti kiasi gani ili wote waweze kuongea lugha moja na kuwa rahisi katika utekelezaji wa bajeti yao ambayo inatakiwa isimamie uzalishaji na matumizi ya vipimo katika viwanda, hivyo sura ya viwanda lazima ionekane katika vipimo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment