Na Robert Hokororo- OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewataka wananchi kutobeza mafanikio yaliyopatikana katika Muungano na kwamba hatakuwa mpole kwa wale wote watakaojaribu kuuchezea Muungano.
Dkt. Mpango alisema hayo Aprili 26, 2021 wakati akifungua Kongamano la miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika Ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.
Alisema zipo faida nyingi zilizoonekana wazi na sile zisizoonekana katika Muungano na hivyo kuufanya kuzidi kuimarika.
“Sehemu kubwa ya Watanzania walizaliwa baada ya Muungano mwaka 1964 na kwa sasa vijana ndiyo kundi kubwa la jamii hiyo hapa nchini hivyo kwa kutambua wingi huo ndio maana jitihada zinafanyika ili kukuza uelewa na ufahamu wa historia na matukio muhimu ya Taifa,” alisema.
Dkt. Mpango aliongeza kuwa Muungano huu ni wa watu hivyo ni Muungano unaoishi ili kutimiza matakwa na malengo ya wananchi wake na licha ya mafanikio mengi yaliyopatikana zilikuwepo pia changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kwa nyakati tofauti na kufanyiwa kazi.
Pia alisisitiza kuwa changamoto hizo hazimaanishi kuwa Muungano wetu sio imara au hauna manufaa kwa wananch bali jambo la kufurahisha ni kwamba Serikali za pande mbili zimekuwa zikibainisha changamoto hizo na kufanya jitihada ili kuzipatia ufumbuzi.
Kwa upande mwingine alizitaja faida ambazo zimepatikana kipindi cha miaka 57 ya Muungano kwa pande zote mbili kuwa ni pamoja na kuimarika kwa udugu wa damu miongoni mwa wananchi,kudumu kwa umoja na mshikamano wa kitaifa.
Faida nyingine ni kuimarika kwa ulinzi na usalama, kukua na kuimarika kwa biashara na shughuli nyingine za kiuchumi na fursa ya kutumia rasilimali zilizopo kwa pamoja ikiwemo ardhi na bahari.
Alisisitiza Serikali za pande mbili chini ya uongozi wa Awamu ya Sita Bara na Awamu ya Nane Zanzibar zimeweka suala la kuimarisha Muungano kuwa ni moja ya vipaumbele vyake na hivyo zinaendelea kushirikiana kwa pamoja kuhuisha na kudumisha muungano.
Aliongeza kuwa amemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Selemani Jafo kumpatia taarifa ya kongamano hilo na mapendekezo yake ili ayafanyie kazi katika kuimarisha utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Wakati huo huo, alisema kuwa maadhimisho yamekuwa yakifanyika kwa shughuli mbalimbali lakini mwaka huu kutokana na kifo cha Hayati Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli waliamua badala ya sherehe lifanyike kongamano. Kwa busara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhe. Samia Suluhu Hassan kuamua lifanyike hivi aliagiza fedha zile kugawanywa kwenda pande zote mbili za muungano na kila upande utaamua namna ya kuzitumia kwa shughuli za muungano,”
Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo alisema Muungano huu umejenga misingi endelevu ya undugu na mshikamano baina ya watu wa pande zote mbili.
Jafo alisema kuwa pande mbili za Muungano zimejenga mifumo ya kuendesha Serikali zake kwa uwazi chini ya misingi ya demokrasia na utawala bora.
Aliongeza kuwa misingi hiyo imeimarika kutokana na uelewa mzuri wa dhana ya uwajibikaji kwa Viongozi wa ngazi zote nchini. Vilevile, ndani ya Muungano, kumekuwa na faida nyingi za kiuchumi kisiasa na kijamii zinazotokana na Muungano wetu, ambazo wananchi wa pande mbili za Muungano wameendelea kunufaika nazo.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, ni matumaini yangu kuwa kwa kupitia Kongamano hili Watanzania wataelewa historia, umuhimu na faida za Muungano wetu adhimu kisiasa, kiuchumi na kijamii ili waweze kuendelea kuuenzi kama tunu muhimu ya nchi yetu. Aidha, watawezeshwa kufahamu fursa zilizopo katika Muungano na kuzitumia ili kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa,”alisema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment