Baraza La Mawaziri La Kisekta La Afya La Ahidi Kuendelea Kushirikiana Katika Kukabiliana Na Changamoto Za Afya


Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya ngazi ya Mawaziri uliofanyika leo katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania; umekubaliana na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya katika Jumuiya.

Mkutano huu uliotimishwa  leo tarehe 23 Aprili 2021, umefanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Aprili 2021, ulikuwa na lengo la kufanya mapitio ya hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na la Kisekta, sambamba na kuibua maeneo mapya yanayohitajika kupewa kipaumbele kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati za Wataalamu.

Mkutano huu uliokuwa ukiongozwa na Mhe. Mutahi Kagwe Waziri wa Afya wa Kenya ambale pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, pamoja na masuala mengine umepitia kujadili na kutoa maelekezo katika kutatua changamoto mbalimbali, zinazokwamisha utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Korona (UVIKO-19), na usalama wa dawa na chakula katika Jumuiya.

Kila Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa nyakati tofauti katika mkutano huo imeeleza utayari wake wa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati na mipango mbalimbali waliyokubaliana kuitumia katika kutatua changamoto za sekta ya afya.

Mkutano huu umehudhuriwa na Mawaziri kutoka Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia masuala ya Afya. Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy O. Gwajima (Mb)


from MPEKUZI

Comments