Mahakama kuu ya kanda ya Iringa iliyofanya kikao chake mkoani Njombe imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa Watu 5 wa kijiji cha Usalule kilichopo wilayani Wanging’ombe mkoani humo kwa kosa la kula njama na kushirikiana kutekeleza mauaji ya Alice Mtokoma( 56 ) mkazi wa kijiji cha Usalule huku sababu kubwa ikiwa ni kulipiza kisasi .
Washtakiwa James Msumule almaarufu Jembe, Emmanuel Ngailo,Izack Ngailo,Anitha Mbwilo na Upendo mligo ambao ni wakazi wa kijiji cha Usalule wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuuua kwa kukusudia chini ya kifungu namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019 .
Wakisoma shauri la namba 84 ya mwaka 2014 mbele ya jaji wa mahakama kuu , jaji Firmin Matogolo mawakili wa serikali Matiko Nyengelo pamoja na Andrew Mandwa wamesema mnamo tarehe 13 mwezi wa tano mwaka 2012 katika kijiji cha usalule washtakiwa walimuua Alice Mtokoma kwa madai ya kulipiza kisasi baada ya kumtuhumu marehemu Alice kuwa alihusika na kifo cha mume wa mshatakiwa Upendo Mligo.
Mahakama imeelezwa kwamba mara baada ya Mume wa Upendo kufariki dunia ,Upendo kwa kushirikiana na mama mkwe wake anaejulikana kwa jina la Anita Mbwilo walikwenda kwa mganga ili kujua aliyemuua ndugu yao ,kwa madai kwamba hakufa kifo cha kawaida na kisha kuelezwa kwamba aliyehusika na kifo ni Alice Mtokoma ambaye ni mke mwenza na Anita Mbwilo.
Baada ya mganga kuwatajia mhusika ndipo Upendo Mligo na Anita Mbwilo wakala njama na kuwatafuta James Msumule almarufu Jembe , Emmanuel Ngailo Na Izack Ngailo na kisha kuwapa fedha kiasi cha sh. laki tatu ili kutekeleza mauaji ya Alice Mtokoma .
Akisoma adhabu jaji Firmin Matogolo amebainisha kuwa washtakiwa wamekutwa na kosa la mauaji ya kukusudia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa adhabu iliyotolewa chini ya kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya 2019 ikisomwa pamoja na kifungu namba 322 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 marejeo ya mwaka 2019.
Upande wa utetezi wa kesi hii umeongozwa na mawakili Frank Ngafunika, Musa Mhagama ,Tunsume Angumbwike,Innocent Kibadu pamoja naye Octavian Mbungani.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment