Balozi Brigedia Jenerali Ibuge: Tuendelee Kudumisha Mahusiano ya Kidiplomasia na Biashara.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge amehimiza Ofisi za Balozi zinazoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya Nchi kuendelea kukuza na kudumisha ushirikiano wa Kidiplomasia na biashara katika maeneo yao ya uwakilishi. Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amesema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Fatma M. Rajab na Balozi wa Tanzania nchini Oman Mhe. Abdallah Abas Kilima.

“Mnadhamana na jukumu kubwa la kuendelelea kudumisha na kukuza mahusiano ya kidiplomasia na biashara katika maeneo yenu ya uwakilishi ili kuendelea kuvutia kwa uwingi wawekezaji na watalii nchini. Jukumu letu la kutumikia wananchi wa Tanzania tulifanye kwa moyo, kujituma, maarifa na uzalendo”. Amesema Balozi Brigedia Jenerali Ibuge.

Balozi Brigedia Jenerali Ibuge vilevile ameeleza dhamira ya Wizara ya kuendeleza viwanja vya Serikali vilivyopo maeneo mbalimbali nje ya nchi ili viweze kuiingizia Serikali mapato na kuipunguzia matumizi yanayotokana na gharama za pango la ofisi na makazi kwa watumishi wanaofanya kazi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Balozi Abdallah Kilima na Fatma Rajab kwa nyakati tofauti wameishukuru Wizara na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano mzuri wanaoendelea kuupata na kuahidi kuwa wataendelea kufanyakazi kwa bidii na weledi katika kulinda na kutetea maslahi ya nchi na kuleta manufaa kwa nchi. 



from MPEKUZI

Comments