Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amewatoa hofu wakazi wa Siha kuwa serikali ipo makini kuwadhibiti nzige waliovamia maeneo ya Tarafa ya Ngare Nairobi jana jioni na kuwa tayari leo ndege imenyunyiza kiuatilifu kuwadhibiti.
Waziri Mkenda amesema hayo jana (24.02.2021) alipotembelea Tarafa ya Siha Magharibi kujionea mahala ambapo nzige walivamia jana hali iliyosababisha hofu miongoni mwa wakulima wa Siha.
“Wananchi msiwe na taharuki nzige wote tutawamaliza na kazi imeanza jana kuwapuliza kiuatilifu kwa kutumia ndege inayomwaga sumu ” alisema Prof. Mkenda
Waziri huyo aewaeleza wakulima wa Siha kuwa wizara yake inafuatilia kwa karibu maeneo yote endapo zige wataonekana basi waangamizwe na kuwa ndege ipo na viuatilifu .
Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amesema hajaridhishwa na kitendo cha shirika la Kudhibiti Ndege wa Jangwani kumpeleka rubani wa ndege iliyopo Moshi nchini Kenya na kuacha Tanzania ikikosa uhakika wa ndege hatua inayoweza leta madhara endapo nzige wataendelea kusambaa.
“Sijafurahishwa na kitendo cha ndege yetu kupaki Moshi halafu rubani shirika la Kupambana na Nzige wa Jangwani wamempeleka Kenya wakati Tanzania ni want wanachama na michango tumelipia yote” alisema Prof. Mkenda.
Ili kuwa na uhakika wa kupambana na visumbufu vya mimea Waziri Mkenda amesema wizar akatika bajeti ya mwaka 2021/22 itatenga fedha za kuanzisha idara maalum itakayoitwa Kilimo Anga na kuipatia vifaa ikiwemo ndege (drones) ili kutumia kuangamiza wadudu kama nzige, kweleakwelea na wengine.
Waziri Mkenda aliongeza kuwa wizara yake itachukua hatua za makini kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuahikikisha kuna usalama na uhakika wa chakula hivyo ” hatutaki nzige watutoe kwenye mstari, tutawateketeza wote mahala walipo” alisema Waziri huyo wa Kilimo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Siha Onesmo Buswelu alisema makundi ya nzige yalionekana jana jioni kwenye mashamba ya Nanai, Nafco, Felisian kwenye kata ya Ngare nairobi.
Buswelu amesema wanashukuru serikali kuwa kutoa ndege ambayo leo imepulizia dawa kwenye mashamba hayo na kuwa wakulima wanaimani kuwa mazao yao hayataathirika na nzige.
Aisha mkulima Said Mohamed Msuya wa West Kilimanjaro akizungumia uwepo wa nzige alisema walipata hofu kuwaona kwani mazao yao yatakuwa hatarini kuliwa.
Msuya alisema “tulipata hofu jana kuona kundi la nzige wakiingia hapa kijiji cha Nanai lakini asubuhi leo tumeona Waziri wa Kilimo Mkenda yupo kututembelea hatua iliyotutia moyo kuwa serikali inatujali”
Prof Mkenda akiambatana na Naibu Waziri Hussein Bashe leo pia watatembelea wilaya ya Simanjiro kukagua hali ya udhibiti wa makundi ya nzige baada ya jana ndege kupuliza kiuatilifu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment