Utambuaji Wamiliki Wa Majengo Uende Sambamba Na Wadaiwa Kodi Ya Ardhi- Naibu Waziri Dkt Mabula


Na Munir Shemweta, WANMM SONGWE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametaka zoezi la utambuzi wa wamiliki wa nyumba liende sambamba na kutambua viwanja visivyolipiwa kodi ya pango la ardhi.


Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana tarehe 22 Februari 2021 wakati akizungumza na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Songwe pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi wakati akiwa katika ziara ya siku moja kukakua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi.


Alisema, ni vyema zoezi la kutambua wamiliki wa nyumba linalosimamiwa na TAMISEMI kupitia watendaji wake wa mitaa na vijiji likaenda sambamba na kutambua viwanja visivyolipiwa kodi pamoja na wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa mazoezi hayo yana lengo la kuingizia serikali mapato.


” Hakuna maana kuchukua kodi ya jengo na kuacha kodi ya kiwanja maana kodi zote hizo zina lengo la kukusanya mapato ya serikali yatakayosaidia katika kuendesha miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati” alisema Dkt Mabula.


Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinafikia asilimia 71 ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kufikia Machi mwaka na kwa halmashauri  itakayoshindwa kufikia kiwango hicho wakuu wa idara au Maafisa Ardhi Wateule watatakiwa kujitathamini kama wanaweza kuendelea na nyadhifa zao. 


Alisema, mkoa wa Songwe uko nyuma katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi na kufikia Januari 2021 umekusanya asilimia 23 tu  ya malengo kiwango alichokieleza kuwa ni kidogo na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri katika mkoa huo kuhakikisha wanasimamia idara za ardhi kwa lengo la kuongeza kasi ya makusanyo.


“Wakurugenzi lazima wajue mapato ya sekta ya ardhi maana halmashauri nyingi  hazitoe taarifa ya mapato ya sekta ya ardhi katika kamati za fedha za vikao vya madiwani wakati wao ni mamlaka za upangaji”


Akielezea suala la utoaji hati katika mkoa wa Songwe, Naibu Waziri wa Ardhi ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya utoaji hati katika mkoa huo ambapo katika kipindi cha miezi nane mkoa umetoa jumla ya hati 333 idadi aliyoieleza kuwa ni ndogo ukilinganisha na mikoa mingine na kutolea mfano wa mkoa wa Mwanza katika wilaya ya Ilemela kwamba watendaji wake wamejipanga ambapo kwa mwezi mmoja wanatoa jumla ya hati 350.  


Aliagiza kila halmashauri katika mkoa wa Songwe itoe hati hansini kila mwezi sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa kumilikishwa ardhi na kubainisha kuwa ni aibu kwa mkoa wa Songwe kupima asilimia 1.1 ya eneo la mkoa huo.


Awali Mbunge wa Jimbo la Songwe Philipo Mulugo alisema kasi ndogo ya utoaji hati katika mkoa wa Songwe inachangiwa na watendaji wa sekta hiyo na kujitolea mfano yeye mwenyewe kuwa ilimchukua muda miaka mitatu kufuatilia hati yake mpaka pale alipofikisha suala lake kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi


Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwengela alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa mkoa wake utaanza mara moja kuyafanyia kazi maagizo yake na kwa kuanzia atataka kila mwezi katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa taarifa ya masuala ya ardhi ikiwemo makusanyo ya kodi ya pango la ardhi iwasilishwe na Ofisi ya Ardhi mkoa.




from MPEKUZI

Comments