Serikali Wilayani Songea Yatoa Saa 24 Kwa Wafanyabiashara Waliogoma Kurudisha Huduma


 SERIKALI wilayani Songea mkoani Ruvuma imewaagiza wafanyabiashara na wasafirishaji abiria waliogoma kurudisha huduma zao ndani ya saa 24 kuanzia saa tisa alasiri Februari 22,2021.


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Songea Cosmas Nshenye akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea, amesema kufuatia mgomo unaoendelea amemwagiza Afisa LATRA kufuta mara moja route ya mabasi yote yanayotoa huduma ya usafirishaji kuanzia Songea mjini hadi Mbinga mjini.


Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa wafanyabiashara wote wenye nia ya kutoa huduma za usafirishaji abiria kutoka Songea mjini hadi Mbinga waombe mara moja kufanya shughuli za usafirishaji katika route hiyo.


Amesema serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa route nyingine za usafirishaji ili kuona ufanisi wake katika kuhudumia wananchi.


“Tuna taarifa kupitia vikao vya wafanyabiashara vilivyofanyika hivi karibuni kuwepo kwa matamshi ya lugha za matusi,uchochezi na uvunjifu wa amani na kuhujumu mipango ya serikali katika kutoa huduma kwa wananchi,hivyo naliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi mara moja na kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wahusika wote watakaobainika kuhusika na vitendo  hivyo’’,alisisitiza Mkuu wa Wilaya.


Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ameliagiza Jeshi la polisi  na LATRA kuweka mpango mbadala wa haraka wa utatuzi wa suala la usafiri katika kurudisha huduma za usafiri ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi.


Mkuu wa Wilaya pia amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na LATRA kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria za Leseni ikiwemo kuwanyang’anya leseni za biashara wahusika wote watakaokaidi maelekezo ya kurudi kazini na kufungua biashara zao ndani ya saa 24 kuanzia saa tisa alasiri Februari 22,2021.


Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia matumizi ya stendi ya Mfaranyaki kama ilivyoamiriwa kupitia vikao vya kisheria vya Baraza la madiwani  la Manispaa ya Songea kwa ajili ya matumizi ya usafiri wa daladala na sio vinginevyo.


Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 22,2021




from MPEKUZI

Comments