Serikali imesema imechukua hatua za kutumia ndege kunyunyiza viuatilifu (sumu) ili kuua makundi ya nzige wa jangwani ambao wamevamia maeneo ya wilaya za Simanjiro na Longido na kuhatarisha ustawi wa mazao na malisho ya mifugo kwenye maeneo hayo.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda jana (21.02.2021) ametembelea eneo la wilaya ya Longido ambalo limevamiwa na nzige wa jangwani ambapo amesema kuwa kuanzia kesho ndege maalum itafanya kazi kupulizia viuatilifu kuua nzige hao.
Prof. Mkenda amewaeleza wananchi na Viongozi kuwa wasiwe na hofu nzige wote watadhibitiwa kupitia wataalam wa Wizara ya Kilimo waliopo kwenye maeneo yote yenye dalili za uwepo wa wadudu hao nchini.
“Kuanzia kesho (leo) (22.02.2021) ndege maalum itaanza kazi kupulizia sumu kuua nzige waliovamia maeneo ya Longido na Simanjiro ili wasiendelee kusambaa na kusababisha maafa” alisema Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema tayari wataalam wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu (TPRI) wapo wilayani Longido na Simanjiro wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake Dkt. Efrem Njau kwa kazi ya kudhibiti wadudu hao waharibifu wa mazao ya kilimo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutokota wala kula nzige watakaokuwa wameuwawa na viuatilifu (sumu) kwenye maeneo yote ambapo ndege hiyo itapita kuua nzige kwani viuatilifu hivyo vinaweza kuwa na madhara kwa binadamu.
Pili, ameagiza wataalam wa kilimo na watendaji wa vijiji na kata kutoa taarifa kwa wananchi juu ya uwepo wa kazi ya kuua nzige hivyo wasiwe na hofu watakapoona ndege inaruka chini kwenye maeneo .
“Wananchi wakiona nzige wameanguka chini wamekufa wasiwachukue au kula kwa kuwa wengi watakuwa wamekufa kwa sumu” alisisitiza Prof. Mkenda
Waziri huyo wa kilimo amesisitiza kuwa serikali itahakikisha mazao ya wakulima na malisho ya mifugo hayaharibiwi na nzige ndio maana ametembelea eneo hilo la Longido ambapo amebainisha mafanikio ya kuwadhibiti tangu walipoingia nchini mwezi Januari mwaka huu kwenye baadhi ya maeneo.
Alisema tangu kuripotiwa na kuthibitika kuwepo kwa nzige wa jangwani haoa nchini wizara imefanikiwa kudhibiti kundi la nzige waliongia mwezi Januari 2021 kwa kuwanyunyuzia sumu aina ya Fenitrothion kwa kutumia ndege mnamo tarehe 10 na 16 Januari mwaka huu.
Prof. Mkenda amesema nzige wa jangwani wana athari kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na malisho ya mifugo na kundi moja la nzige lina uwezo wa kuruka bila kutua kwa umbali wa kilometa 150 Kwa siku.
Aidha, nzige wana uwezo wa kula Sawa na uzito wake Kwa siku ambapo kundi moja la nzige linaweza kuwa na wastani wa nzige milioni 40 kwenye eneo la kilometa moja za mraba alisema Waziri Mkenda .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Jumaa Mhina ametoa agizo shule zote za msingi na sekondari kwenye maeneo ambapo ndege itapuliza viuatilifu kusitisha masomo kwa muda wa siku 4 kuanzia kesho ili kudhidhibi watoto wasije wakapata madhara endapo watashika au kuchezea nzige watakaokufa.
Anaye Mbunge wa Longido Dkt. Steven Lemomo Kiruswa ameiomba serikali iharakishe kupulizia viuatilifu ili nzige wasije leta madhara kwa mifugo na wakulima kwenye maeneo ya Longido na kwingineko. .
” Leo ni siku ya tatu nzige wameingia Longido, tunaomba jitihada za wataalam wa TPRI kuwadhibiti ili wasilete madhara kwetu sisi wafugaji tunaotegemea nyasi kwa malisho” alisema Mbunge Kiruswa.
Mwisho.
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment