Na Mwandishi wetu- Dodoma
Wizara ya Kilimo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)zimetiliana saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya kilimo ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuzalisha kwa tija ili kuiliwezesha Taifa kuwa na ziada ya chakula na mazao ya biashara.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya Februari 26, 2021 makao makuu ya JKT wilayani Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kutiliana saini mkataba huo kati ya Wizara hiyo na JKT kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya pande hizo.
“Makubaliano haya ni ya miaka mitano na baadhi ya maeneo ya ushirikiano ni pamoja na; kuimarisha teknolojia bora za uzalishaji zinazoendana na wakati,Kujenga uwezo wa kusambaza teknolojia za kilimo, Huduma za umwagiliaji, Utafutaji masoko, huduma za usimamizi wa mazao ikiwemo kuongeza thamani mazao ikiwemo mpunga utakaozalishwa kupitia kikosi cha Chita Kilombero mkoani Morogoro”, alisisitiza Kusaya.
Akifafanua Bw. Kusaya amesema kuwa makubaliano hayo yatawezesha Wizara ya Kilimo na JKT kufanya tafiti za pamoja,kuanzisha mpango wa pamoja wa usambazaji wa taarifa za kilimo ikiwemo teknolojia,kubadilishana taarifa za masoko, kufanya usimamizi na tathmini ya pamoja.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Charles Mbuge amepongeza ushirikiano uliopo kati ya JKT na Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).
Aidha, Meja Jenerali Mbuge ameleza kuwa Jeshi hilo ni chombo pekee ambacho kikitumika katika kukuza sekta ya kilimo kitaleta matokeo makubwa katika sekta ya kilimo ambapo aliahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyopangwa yanafikiwa.
“ JKT katika mwaka 2019/ 2020 na 2020/2021 imeanzisha kilimo cha kimkakati katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupitia kikosi cha Chita wilayani Kilombero mkoani Morogoro ambapo inazalisha mpunga kwenye eneo la ekari 2500 na baadae ekari 12,500 ambapo lengo ni kuongeza uzalishaji mara mbili zaidi.
Aliongeza kuwa JKT inatumaini kuwa Wizara ya Kilimo itasaidia katika kuwezesha ujenzi wa maghala katika vikosi vya Jeshi hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Tawi la Utawala JKT ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi JKT Kanali Hassan Mabena amesema kuwa wamechukua hatua za makusudi katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kutimiza azma ya Taifa kujitegemea kwa chakula na pia kuzalisha mazao ya biashara.
Aidha, Kanali Mabena amesema kuwa JKT imekuwa na ushirikiano mzuri na TARI, ASA na Taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo.
Aliongeza kuwa katika kuimarisha uzalishaji JKT imenunua matrekta 15 pamoja na zana nyingine za kilimo kwa lengo la kuzalisha kwa tija.
Makubaliano kati ya JKT na Wizara ya Kilimo yanatajwa kuwa chachu ya ukuaji wa sekta hiyo hapa nchini na kuwezesha Taifa kujitegemea na kuuza ziada itakayozalishwa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment