ACT- Wazalendo Wapata Mrithi wa Maalim Seif


Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kimeshapendekeza jina la mwanachama atakayemrithi  Maalim Seif Sharif Hamad umakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Maalim Seif alifariki dunia Februari 17 mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).


Zitto Kabwe ameeleza hayo jana  Jumamosi Februari 27,2021 wakati wa hitma ya kumuombea Maalim Seif katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini hapa.

Katika maelezo yake, Zitto alisema kilichobaki ni kusubiri uteuzi utakaofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa mujibu wa Katiba.

“Bahati nzuri, Maalim Seif alikuwa ni kiongozi. Alijua kuna siku Mungu atamchukua kwa sababu sisi sote lazima turejee kwa  Mungu kama tulivyoambiwa katika mafunzo ya dini.

“Kwa hiyo aliacha maelekezo ya nini kitokee iwapo atatangulia mbele ya haki. Namshukuru Mungu kwamba viongozi wa chama wamefuata yale maelekezo yake kwa namna ambayo alivyotuelekeza sasa umebaki wajibu wa Dk Mwinyi kuyatekeleza hayo,” alisema Zitto.

Zitto amesema chama hicho kinaamini mwanachama aliyependekezwa ana uwezo wa  kusimamia maridhiano na haki za Wazanzibari kama ambavyo Maalim Seif alivyokuwa akifanya.



from MPEKUZI

Comments