UCSAF Kufikisha Huduma Za Mawasiliano Maeneo Ya Mipakani Ili Kulinda Usalama Wa Nchi


•UCSAF yasaini mikataba ya kupeleka huduma za mawasiliano vijijini kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano ya simu
•Zaidi ya watanzania laki saba kufikiwa na huduma za mawasiliano baada ya miradi kukamilika
•Waziri atoa onyo kwa makampuni ya simu yanayotoa taarifa za wateja asema watachukuliwa sheria


Na Celina Mwakabwale, Kitengo cha Mawasiliano UCSAF

Mtendaji Mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema Mfuko huo umeanza kutekeleza miradi ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya mipakani kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma hiyo muhimu, lakini pia kwa lengo la kuhakikisha usalama wa nchi.


Ameyasema hayo wakati wa halfa ya utiaji saini mikataba mitatu iliyosainiwa kati ya UCSAF na makampuni ya simu ya Vodacom, Artel na Tigo ambayo inapeleka huduma za mawasiliano katika Vijiji 173 vilivyo katika Kata 61. 


Kampuni ya Airtel Tanzania inapaleka mawasiliano katika Vijiji 73 kutoka katika kata 25 kwa ruzuku ya shilingi bilioni 2.7, kampuni ya Vodacom inapeleka mawasiliano katika vijiji 63 kwa ruzuku ya shilingi bilioni 2.6 na kampuni ya tigo itapeleka mawasiliano katika Vijiji 31 katika kata 13 kwa ruzuku ya bilioni 1.5


Tukio hilo la utiaji saini limeshuhudiwa na mgeni rasmi Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile aliyeambatana na Naibu Waziri Mhandisi Andrea Kundo, Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Jim Yohazi pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo. 


Dkt Ndugulile ameipongeza UCSAF na kuongeza kuwa utiaji saini huo ni kielelezo cha ushirikiano mzuri baina ya Serikali na Makampuni binafsi, na kusema kuwa hatua hiyo ni ya kupongezwa. Aidha Dkt Ndugulile imeitaka UCSAF kwa kushirikiana na makampuni ya simu kuongeza wigo wa upelekaji huduma za mawasiliano ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.


Wakati huo huo Dkt Ndugulile ametoa onyo kwa makampuni ya simu ambayo baadhi ya watumishi wake wamekuwa wakitoa taarifa za wateja bila kufuata utaratibu huku akiitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatilia na kampuni itakayobainika itachukuliwa hatua za kisheria.


Nae Naibu Waziri, Mhandisi Andrea Kundo amesema mahitaji ya mawasiliano yanazidi kuongezeka na ili kukidhi mahitaji hayo, kunahitajika uwekezaji katika kufanya tafiti na uvumbuzi wa teknolojia ambayo inaweza kutumika vizuri nchini kwani mawasiliano yanaenda kuwa moja ya njia kuu za kukuza uchumi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesisitiza kukamilika kwa wakati kwa miradi hiyo na kuwataka wadau hao kutimiza kuzingatia makubalino yaliyofikiwa.


Miradi hiyo mitatu inatekelezwa katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Simiyu, Singida, Tabora, Kagera, Lindi, Geita, Mara na Njombe na baada kukamilika kwake watanzania zaidi ya laki saba watapata huduma za mawasiliano.


Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano- Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF)





from MPEKUZI

Comments