Majaliwa: Wamachinga Ni Muhimu Katika Kukuza Pato La Taifa


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa Waziri Mkuu amesema Wamachinga ni watu muhimu katika kukuza pato la Taifa na takwimu za Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonesha kuwa Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imetengeneza ajira, kukuza uchumi na kuondoa umasikini.

Hivyo, Waziri Mkuu ameziagiza mamlaka zinazohusika na ujenzi wa masoko mazuri unaoendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini wazingatie na waandae miundombinu kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Januari 28, 2021) katika kikao na Viongozi wa Wamachinga Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Sekta hiyo ina jumla ya wajasiriamali milioni 3.1 ambao wameajiriwa ni asilimia 23.4 ya nguvu kazi ya Taifa na imechangia asilimia 27 katika pato la Taifa.

Kauli Mbiu ya Mkutano huo inasema “Wamachinga ni fursa sahihi ya kujenga uchumi”, ambapo, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wake utakuwa ni muarobaini wa changamoto zote zinazowakabili Wamachinga nchini kwani kila mmoja kwa nafasi yake atatimiza wajibu wake ili kuhakikisha wanafanya kazi zao na hivyo kuweza kuchangia ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Amesema anaamini kuwa wadau wote  nchini wataitumia kaulimbiu hiyo katika kuchochea  maendeleo ya wafanyabiashara wadogo kwa kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na hivyo kuwawezesha kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Wamachinga ni watu muhimu sana na wamekuwa suluhisho la mahitaji kwa watu wengi kuanzia wenye kipato cha chini, kati na kipato cha juu, hivyo ametoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kuunga mkono shughuli zao kwa vitendo

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wamachinga wote nchini ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitambulisho maalum vinavyowapa uhalali wa kufanya biashara zao bila bugudha. “Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali inathamini sana mchango mkubwa wa sekta isiyo rasmi katika kuinua uchumi.”

“Wakurugenzi katika Halmashauri zote wahakikishe wanapata takwimu sahihi za Wamachinga ili irahisishe zoezi la utoaji vitambulisho vya biashara  ili kuepuka usumbufu. Ndugu zangu Wamachinga vitambulisho ni muhimu kwani vinakupeni uhalali wa kufanya biashara zenu bila bugudha.”

Amesema hata sekta zilizo rasmi nao wana vitambulisho vinavyowawezesha kupata huduma zao kama waajiriwa. Serikali kupitia Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeamua kutoa vitambulisho rasmi ambayo vitawatambulisha popote nchini na kupata huduma muhimu.

Waziri Mkuu amesema sekta isiyo rasmi imetoa fursa nyingi za ajira ikilinganishwa na wale walioajiriwa katika sekta rasmi. “Kwa kutambua hilo, nitoe wito kwa wamachinga wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.”

Amesema Sekta ya Biashara Ndogo imesaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira nchini kwani imewezesha kila mpenda kazi kwa vijana, wanawake na wahitimu wa ngazi zote kujiajiri ikiwemo wanaohitimu wa elimu ya msingi, sekondari, ngazi ya kati na hata vyuo vikuu.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kushughulikia changamoto zinazowakabili Wamachinga ikiwa ni pamoja na kuwajengea mazingira bora yatakayowawezesha kufanya biashara zao katika maeneo stahiki.

Waziri Mkuu, ametumia fursa hiyo kuwataka Wamachinga wawe wazalendo na wasikubali kutumika kwa kusaidia mtu mwingine kukwepa kulipa kodi kwa kukubali kupokea bidhaa kutoka katika maduka makubwa bila risiti ya mauzo kitendo ambacho kinasaidia kutolipa kodi, hivyo, aliwataka wasikubali kusaidia wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi wakati wao wanalipa kodi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania, Ernest Matondo Masanja pamoja na mambo mengine alimuomba Waziri Mkuu awasaidia katika kutatua mgogoro uliopo baina ya Wamachinga wa Jiji la Mbeya na uongozi wa jiji hilo kwani tangu mwaka 2018 wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Pia, Mwenyekiti huyo amemuomba Waziri Mkuu awasaidie Serikali ifanye maboresho katika mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri ili na wakinababa nao waweze kunufaika na mikopo hiyo. Serikali imetenga asilimia 10 ya mapato ya kila Halmashauri kwa ajili ya kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake, vijana na wenyeulemavu.


from MPEKUZI

Comments