Rais Dkt John Magufuli leo ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga mkoani Tabora, – Revocatus Kuuli.
Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kufuatia tuhuma za kujitwalia ardhi ya Wananchi bila kufuata utaratibu, utendaji kazi usioridhisha na ubadhilifu wa fedha za maduhuli ya Serikali zinazomkabili Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo aliposimama kuwasalimu Wananchi wa Igunga wakati akiwa safarini, ambapo Wananchi na Viongozi wa Tabora wamepata fursa ya kueleza kero zao.
Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Phillemon Sengati kuteua mtumishi mwadilifu atakayekaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga mpaka hapo uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji mwingine atakayeendana na kasi ya Serikali ya awamu ya Tano utakapofanyika.
Rais Magufuli amesema pamoja na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, anazo taarifa nyingi za dosari za Kuuli na aliishamuonya juu ya vitendo vyake vya kuwadhulumu wananchi wakiwemo wanawake na hivyo Serikali anayoiongoza haiwezi kumvumilia kiongozi wa namna hiyo.
Wakati huo huo Rais Magufuli amewashukuru wananchi wa Igunga na Watanzania kwa ujumla kwa kumchagua kwa kura nyingi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili na ameahidi kuwatumikia kwa uwezo wake wote.
Amewapongeza wananchi wa Tabora, Igunga na Nzega kwa kupata maji kutoka Ziwa Victoria na amewasihi kutumia maji hayo vizuri kwa manufaa yao.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment