Wanafunzi Wanusurika Bweni la Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto Jijini Mwanza Likiteketea Kwa Moto
BWENI la Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto iliyopo wilayani Ilemela limeteketea kwa moto, huku wanafunzi zaidi 100 wakinusurika katika tukio hilo.
Mkuu wa Sekondari ya Wasichana Loreto, Basilisa Materu ameeleza alivyopata wakati mgumu kuwazuia wanafunzi wasifuate vifaa vyao wakati bweni lilipoteketea kwa moto ili kuokoa uhai wao.Shule hiyo iliyopo Ilemela, ina bweni moja la ghorofa tatu likiwa na uwezo wa kutunza wanafunzi 500 na sehemu ya juu kabisa inayotumiwa na wanafunzi 130 wa kidato cha kwanza ndilo lililoungua.
Bweni hilo liliungua saa 12:20 jioni ya Novemba 21 na kuteketeza vifaa vyote vya wanafunzi ingawa hakuna aliyedhurika.
Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji waliwahi na kuudhibiti moto huo kabla ya kusambaa.
Basilisa, mtawa wa Kanisa Katoliki linalomiliki shule hiyo alisema moto huo ulizuka wakati wanafunzi wakiwa wanakula na wengine kwenye sala ya jioni.
“Nilipata wakati mgumu kuwazuia watoto walipotaka kufuata vifaa vyao. Mwanzo hawakunielewa lakini baadaye. Niliwapeleka uwanjani na kuwakalisha chini,” alisema mtawa huyo.
Baada ya kuwapeleka uwanjani alisema “tukaanza kuomba rozari na sala nyingi baada ya muda viongozi wa Serikali na Jeshi la Zimamoto walifika na kuuzima moto huo,” alisema.
Licha ya vifaa vya wanafunzi kuteketea, m kuu huyo alisema shule itawanunulia sare na vifaa vingine bila kuwahusisha wazazi
“Tutajibana hivyohivyo. Niwatoe hofu wazazi, wanafunzi wapo salama na hatutawapa mzigo wa kununua sare,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk Severine Lalika alisema ameziagiza halmashauri kuchangia kuwasaidia wanafunzi hao na taasisi binafsi ziwasiliane na uongozi wa shule kuswasaidia wanafunzi hao .
Alisema “uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha moto huo ni shoti ya umeme. Tutatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha uchunguzi.”
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment