Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali kupitia Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya imesema kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya halijatoa azimio lolote kuhusu Tanzania kupitia kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Bunge hilo.
Akizungumza mapema leo kupitia televisheni ya Taifa (TBC), Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya Jestus Nyamanga alisema kuwa kuna taarifa za upotoshaji na zisizo na ukweli wowote zinazosambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii zikidai kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya jana Novemba 19 limeazimia kusitisha misaada na mikopo kutoka umoja huo na mashirika yake, kwa nchi ya Tanzania sambamba na kuiwekea vikwazo.
Halikadhalika taarifa hizo za upotoshaji zinadai kwamba Bunge hilo la Umoja wa Ulaya limeazimia kuiwekeza vikwazo Tanzania na kuzuia kuuza bidhaa zake katika nchi za Umoja wa Ulaya.
“Novemba 19 asubuhi hapa Ubeligiji, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya ilikutana katika kikao chake cha kawaida, moja ya masuala yaliyojadiliwa ilihusu Tanzania na hali ilivyo baada ya Uchaguzi Mkuu kukamilika, huu ni utaratibu wa kawaida kabisa wa Kamati hiyo kuijadili nchi ambayo ni mdau wao mkubwa wa maendeleo mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu kukamilika”, alisema Balozi Nyamanga
Balozi Nyamanga alifafanua kuwa kikao hicho ni kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na si Bunge lote na hata hivyo kikao hicho kilitoa nafasi kwa wabunge kutoa mawazo yao na kujadili kuhusu hali ya Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu ambapo ni wabunge watano tu ndio walitoa mawazo yao kati ya wabunge 71 wa Kamati hiyo. Ambapo hilo lina idadi ya wabunge 705 na hivyo halijatoa azimio lolote kuhusu Tanzania.
Alibainisha kuwa pia kuna taarifa ambazo si za kweli zinazoenezwa na watu wenye nia mbaya na Tanzania zikidai kwamba Bunge hilo la Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia Tanzania msaada wa euro milioni 626 ambazo Tanzania inapewa na Umoja wa Ulaya kila mwaka, si kweli kwamba Umoja huo unaipa Tanzania fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Aidha Serikali inaendelea kutekeleza miradi yake mbalimbali.
“Hakuna mjadala wala majadiliano yanayoendelea katika Umoja wa Ulaya wala hakuna azimio lililowekwa na Kamati hiyo ya Bunge, wala kuizuia Tanzania kuuza bidhaa zake katika nchi hizo za Umoja wa Ulaya, hata hivyo naomba niwahakikishie watanzania wenzangu kwamba uhusiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya ni mzuri sana kwa zaidi ya miaka 45 sasa na tunaendelea kushirikiana katika masula mbalimbali yanayohusu maendeleo kwa pande zote mbili”, alisema Balozi Nyamanga.
Mwisho.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment