MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
“Serikali imetoa sh. bilioni 3.02 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Masoko ambacho kimekamilika na kinatoa huduma; kituo cha afya cha Pande kinatoa huduma; kituo cha afya cha Tingi kinatoa huduma; kituo cha afya cha Somanga kinatoa huduma na kituo cha afya cha Nanjilinji ambacho ujenzi wake uko kwenye hatua ya ukamilishaji.”
Ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Oktoba 22, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Ilulu Njianne katika kata ya Tingi na Kivinje kwenye mikutano iliyofanyika wilayani Kilwa, mkoani Lindi.
Akielezea kuhusu uboreshaji wa afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 403 zimetolewa na Serikali kuboresha hospitali ya wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa duka la dawa na jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya Kinyonga. Alisema ujenzi wake upo katika hatua za ukamilishaji.
Kuhusu uboreshaji wa zahanati, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 164.7 zimetolewa kwa uboreshaji wa zahanati za Rushungi na Songomnara. Kwenye ununuzi wa dawa, alisema: “Shilingi bilioni 1.43 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo wastani wa fedha za ununuzi wa dawa kwa mwezi ni shilingi milioni 23.9.”
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Lindi kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge wa majimbo ya Kilwa Kaskazini, Bw. Francis Ndulane na Bw. Ally Kasinge (Kilwa Kusini), pamoja na wagombea udiwani wa kata za majimbo hayo kwa tiketi ya CCM.
Akielezea kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 7.5 zimetolewa kwa miradi mikubwa ya maji ikwemo mradi wa utafiti wa maji na uchimbaji visima katika vijiji 19; Mradi wa kuboresha huduma ya Maji Kilwa Masoko, ujenzi wa mabomba Somanga na Pande na ujenzi wa mabomba Njia Nne.
“Fedha hizo zimetumika kufanya ukarabati wa mradi wa maji Kipatimu, Ukarabati wa mradi wa maji Mandawa, mradi wa maji ya bomba na uvunaji wa maji ya mvua Mingumbi-Miteja, ukarabati wa mradi wa maji Kijiji cha Kipindimbi, ukarabati wa pampu za mkono 25 katika vijiji 12 vya Kilwa pamoja na Mradi wa Maji ya Bomba Shule ya Sekondari Kinjumbi,” alisema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment