Na.WAMJW-Dodoma.
SERIKALI imesema haitasita kumchukulia hatua Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya atakayebainika kushindwa kusimamia fedha za Mradi wa Boresha Macho.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Dkt.Ntuli Kapologwe jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Boresha Macho unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Uingereza(UKAID).
Dkt.Kapologwe amesema mradi huo unagharimu Shilingi za kitanzania Bilioni 6 “lazima kuwepo na usimamizi mkubwa wa fedha hizo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”.
Ameendelea kusisitiza kuwa kama kuna Mganga mkuu ambaye atashindwa kusimamia vizuri fedha za mradi huo atajieleza kwanini hawezi kusimamia.
“Tuchukue mradi huu kama mtoto wetu na malengo tuliyoweka lazima yafanikiwe,hatutamvumilia mtu yeyote aidha anatoka shirika lisilo la kiserikali au serikalini ambaye hatatekeleza inavyotakiwa, kwasababi hizi fedha zimeletwa kwa ajili ya watanzania na wanapaswa kunufaika na kila uwekezaji unaofanywa kwenye macho,”Amesema Dkt.Kapologwe.
Aidha, Dkt. Kapologwe ameeleza kuwa suala la ubora wa kazi itakayofanyika ni la msingi ili mradi ufanyike kwa malengo yaliyokusudiwa huku akisema pale itakapobainika mradi hautekelezwi ipasavyo serikali haitasita kuchukua hatua.
“Kila senti moja ambayo imetolewa kwa ajili ya mradi huu lazima iwafikie walengwa ambao ni wananchi, sisi Tamisemi na Wizara ya Afya tutafanya ufuatiliaji wa karibu ili kuona kama kuna thamani ya fedha kwenye utekelezaji wa mradi huu, Sh.Bilioni sita za mradi tunataka tuone vitu,”Amesema.
Hata hivyo amesema serikali imekuwa ikiendelea kuimarisha huduma za afya kwa wananchi ambapo zimeshuka hadi ngazi za kijiji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Afya anayeshughulia magonjwa yasiyo ambukiza, Dkt.James Kiologwe, amesema asilimia moja ya watanzania wanakabiliwa na tatizo la uoni ambao unasababisha kupata upofu.
Hata hivyo, amesema asilimia 75 ya matatizo yanayosababisha upofu yanazuilika na Wizara ya Afya inajivunia kufanya kazi na wadau kuhakikisha idadi hiyo ya watu wanapata tiba ili wasipate upofu.
“Katika ushirikiano huo kuna mambo tunajivunia hadi sasa, tumeweza kuratibu vizuri wadau, tunajua katika viwango vya kimataifa tunatakiwa kuwa na hospitali moja ya kutoa huduma za upasuaji kwa watoto wanaopata matatizo ya macho, tunafurahi hadi sasa kuna hospitali nne ambazo zinauwezo huo,”.
Awali, Meneja Mipango na Mshauri Mwelekezi wa sightsaves Eng. Koronel Kema, amesema mradi huo utagharimu kiasi cha Sh.Bilioni sita na unatarajiwa kupima na kutoa huduma za macho kwa watu 150,000 huku kati yao 13,500 watakaobainika na mtoto wa jicho watafanyiwa upasuaji.
Aidha, amesema mradi huo pia utaongeza uelewa kwa watu 650,000 kuhusu umuhimu wa kupata huduma za macho.
“Mradi utafikia halmashauri tano kati ya tisa za Mkoa wa Morogoro na kwa Mkoa wa Singida Halmashauri zote tisa zitanufaika,”amesema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment