Wafanyabiashara wa Madini Mikononi mwa TAKUKURU


Wafanyabiashara wakubwa saba wa madini ya Tanzanite mkoani Arusha, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kufanya biashara ya madini ya vito kwa njia ya magendo.


Wanatuhumiwa kujihusisha na utoroshwaji wa madini kwenda nje ya nchi na ukwepaji wa kodi, kinyume cha sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na serikali katika biashara hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, katika mkutano na waandishi wa habari jijini hapa jana, aliwataja wafanyabishara hao kuwa ni pamoja na Joel Mollel, maarufu 'Saitoti', meneja wa kampuni ya Gem and Rock Venture ya jijini Arusha na mke wake Caren Mollel ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Asia, Rakesh Kumar Gokhroo anayemiliki kampuni ya kuuza na kununuwa madini ya Colour Clarity jijini.

Wengine ni Daud Saimalie Lairumbe, wakili wa kampuni ya Gem and Rock Venture kutoka Kampuni ya Uwakili ya Northen Law Chambers Advocates & Legal Cunsultants ya jijini Arusha, George Poul Kivuyo, maarufu kwa Lekoo, mchimbaji na mfanyabiashara wa madini na mshiriki wa kibiashara wa Saitoti.

Naiman Mollel, mchimbaji wa madini ya Tanzanite katika mgodi ulioko Mirerani unaomilikiwa na Kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha pamoja na Ezekiel Laizer, mchimbaji na mfanyabiashara wa madini na mshirika wa kibiashara wa Saitoti wa jijini Arusha.

Mkurugenzi huyo alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wafanyabiashara Saitoti na Gokhroo kwa kushirikiana na wenzao hao watano wanatuhumiwa kufanya uchimbaji, ununuzi na usafirishaji haramu wa madini ya Tanzanite kutoka katika migodi ya madini hayo yaliyoko Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Alisema kuwa tuhuma zilizochunguzwa na zinazoendelea kuchunguzwa ni pamoja na watuhumiwa wote kutumia rushwa kuwashawishi baadhi ya watendaji wa serikali kufanikisha azma yao ya kupunguza thamani ya madini husika, hivyo kuikoshesha serikali mapato kwa madini husika kupewa thamani ndogo.

Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakipata madini bila kufuata sheria, kanuni na taratibu na kuyauza nje ya nchi kinyume cha taratibu, hivyo kuendelea kuikosesha serikali mapato stahiki.


from MPEKUZI

Comments