TARI Naliendele Yaagizwa Kutafiti Mbegu Bora Zenye Mavuno Mengi Kwa Wakulima


Wizara ya Kilimo imekiagiza kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele kuongeza kasi ya utafiti wa mbegu bora nyingi za korosho na mazao ya mafuta ili wakulima waweze kuwa uhakika wa mavuno na kuinua kipato cha kaya.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema hayo jana mjini Mtwara alipotembelea kukagua shughuli za utafiti wa mbegu za korosho na mazao ya mafuta katika kituo hicho.

Kusaya amewataka watafiti wa kilimo kujikita katika kuzalisha mbegu bora za korosho kisayansi zenye kutoa mavuno mengi na kumsaidia mkulima kuwa na kipato cha uhakika.

“Bado tunalo deni la kugundua zaidi mbegu bora za mazao mengi tukiwa na lengo baada ya miaka kumi nchi ijitosheleze kwa mahitaji ya mbegu na kupunguza utegemezi toka nje ya nchi” alisisitiza Kusaya

Katibu Mkuu huyo aliwaeleza watafiti hao kuwa wanafanya kazi nzuri na serikali inatambua hilo lakini waongeze jitihada zaidi hususan kwenye upatikanaji wa mbegu nyingi bora za mazao ya mafuta kama ufuta, karanga na alizeti ili kuondoa tatizo la upungufu wa mafuta ya kula.

Aliongeza kusema kwa mwaka nchi inatumia shilingi bilioni 443 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi wakati tunayo ardhi kubwa na bora inayofaa kwa uzalishaji mazao ya mafuta ikiwemo michikichi na ufuta.

“Rais Dkt.John Pombe Magufuli amekwisha agiza na kuiwezesha TARI kupata zaidi ya shilingi bilioni 1.7 mwaka huu kwa ajili ya utafiti wa mazao ya michikichi ili nchi iondokane na upungufu wa mafuta, ni jukumu lenu watafiti kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za ufuta, alizeti na michikichi” alisema Kusaya.

 Lengo la wizara ya kilimo ni kuwa na aina nyingi za mbegu za mazao ikiwemo ufuta ,alizeti, michikichi, karanga na muhogo ili eneo ambalo halistawi korosho basi mkulima apande zao jingine la kumwingizia kipato na uhakika wa chakula alisema Kusaya.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Naliendele Dkt. Fortunus Kapinga alisema wamefanikiwa kugundua aina 54 za mbegu bora za korosho ambazo  zinazaa sana, kuvumilia magonjwa na kustawi maeneo mengi nchini.

Alitaja mafanikio mengine ya kituo hicho ni pamoja na uzalishaji wa mbegu bora za korosho  tani 106 (2017/18), tani 47.5 (2018/19) na tani 111.2 ambapo tayari   tani 82 zimesambazwa nchini katika msimu wa 2019/20.

“Tunatarajia kuzalisha tani 100 za mbegu bora za korosho msimu wa 2020/21 ili tuweze kuzisambaza kwenye mikoa yote 20 ambayo inalima korosho kwa sasa Tanzania” alisema Dkt Kapinga.

Dkt. Kapinga alimweleza Katibu Mkuu Kilimo kuwa lengo la kituo cha utafiti Naliendele ni kufungamanisha zao la korosho na mazao mengine ili kuwa na uhakika wa soko mfano kuzalisha maziwa ya korosho, kubangua korosho,  kutengeneza mvinyo wa korosho, kuzalisha mafuta ya alizeti na karanga nk

“Kwenye mabibo tumegundua unaweza kupata ‘Ethanol’ inayohitajika sana kwenye maabara na tayari Mkemia Mkuu wa Serikali ameithibitisha ubora wake” alisema Dkt.Kapinga .

Kuhusu Programu ya Utafiti  wa Mbegu za Mafuta na Mikunde Dkt. Kapinga alieleza mafanikio kuwa TARI Naliendele imegundua aina 9 za mbegu bora za ufuta,  aina 15 za karanga na aina 3 za alizeti ambazo zina mavuno mengi kwa wakulima.

Katibu Mkuu Kusaya alitembelea pia Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Mtwara ambapo alikipongeza kwa kufundisha wanafunzi na wakulima kwa vitendo kilimo cha zao la korosho kupitia mashamba darasa.

Kusaya aliwisihi watumishi wa chuo hicho kuwa wizara itaendelea kuwajengea uwezo wa kuwafanya wajitegemee zaidi kimapato kwa kuwapatia vifaa ikiwemo trekta na kuboresha miundombinu ya chuo hicho kiweze kuongeza udahili na tija katika mafunzo.

Naye Mkurugenzi wa Mafunzo ,Utafiti na Ugani toka Wizara ya Kilimo Dkt. Wilhem Mafuru alimshukuru Katibu Mkuu kwa jitihada zake za kuboresha utendaji kazi wa vyuo vyote 14 na vituo 4 vya mafunzo ya kilimo kwa kuvipatia fedha ya ukarabati, vifaa vya TEHEMA, magari na pikipiki hali inayoongeza morali kwa watumishi.

“Katibu Mkuu tunakushuru sana  tangu uingie wizarani umekuwa msaada kwa vyuo vya kilimo kwani tayari umeshatembelea vyuo 13 kati ya 14 hali inayotia imani kuwa sasa vinatambulika na vinaboreshwa“ alisema Dkt. Mafuru.

Kwa upande wake Maimuna Yakini akizungumza kwa niaba ya watumishi wa MATI Mtwara alisema anaishukuru serikali kwa kuweza kulipa madeni ya wazabuni kwenye vyuo vya kilimo na pia watumishi hali inayowafanya wawe na maisha mazuri.

“Tunakushuru sana Katibu Mkuu Kusaya kwa kututia moyo tufanye kazi kwa bidii na tunamwombea Mungu amsaidie Mhe.Rais Dkt.Magufuli ashinde uchaguzi ujao ili aendelee kutekeleza malengo yake katika kuinua sekta ya kilimo ikiwemo vyuo vyetu vya mafunzo” alihitimisha Maimuna.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred alisema lengo la wizara  ni kuongeza uzalishaji wa korosho toka tani 300,000 msimu wa 2019/20 hadi tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2023/2024 ambapo msimu huu uzalishaji unatarajia kuwa tani 278,000 za korosho ghafi.

Katibu Mkuu Kusaya amemaliza ziara yake mkoani Mtwara jana ambapo aliweza kushiriki kikao cha kujadili mkakati wa kuvipatia malighafi viwanda vya wabanguaji korosho wa ndani, kutembelea bodi ya korosho kuangalia maandalizi ya ununuzi wa korosho msimu wa 2020/21 na Chama Kikuu cha Ushirika Masasi/Mtwara (MAMCU).


from MPEKUZI

Comments