Takukuru Yakanusha Taarifa Za Upotoshaji Kuhusu Taasisi Hiyokuwabambikizia Wananchi Kesi


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini,[TAKUKURU]imekanushwa Taarifa za kuwabambikiza  wananchi kesi za tuhuma za Rushwa na utakatishaji wa fedha  na baadae kutaifisha fedha za Watuhumiwa  hao kutoka katika akaunti zao za benki.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Septemba,23,2020 jijini Dodoma mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo amesema taarifa hizo si za kweli na zenye nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya wananchi kwa serikali yao.

“Tunapenda umma wa Watanzania utambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi kwa weledi mkubwa na kwamba suala kama hili halijawahi kutokea.

Wananchi wa Tanzania wanalindwa na katiba ya nchi na ndio maana wanapotuhumiwa kwa makossa yoyote yakiwemo ya Rushwa watuhumiwa hao huwa na haki ya kujitetea  ikiwa ni pamoja na kuwa na mawakili”amesema.

Aidha,Bregedia Jenerali Mbungo amesema TAKUKURU inapokuwa imepokea tuhuma ,inafanya uchunguzi ili kupata Ushahidi dhidi ya tuhuma hiyo  ambapo mara baada ya kukamilika  upatikanaji wa  Ushahidi jalada la uchunguzi hupelekwa kwa mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma [DPP] kwa ajili ya mapitio ya Ushahidi na akiridhika na Ushahidi huo ndipo kesi hufunguliwa mahakamani.

“Tuwasihi Wananchi ,watambue kuwa watu ambao wamekuwa wakitoa tuhuma juu ya TAKUKURU au serikali kuwabambikizia kesi wananchi sio za kweli na wana nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya wananchi kwa serikali yao  na wanataka kurudisha nyuma kasi ya mapambano dhidi ya rushwa nchini”amefafanua.

Hivyo,Mkurugenzi mkuu huyo wa TAKUKURU ametoa rai kwa Watanzania wasikubali kudanganywa   na wapuuzie taarifa za aina hiyo .

Kuhusu upokeaji wa Taarifa amesema TAKUKURU imekuwa ikipokea taarifa 100 kwa kila siku nchi nzima za malalamiko na zihusuzo urejeshaji wa fedha kwa wananchi  waliodhurumiwa haki zao  ikiwemo kuingizwa katika mikopo ya riba kubwa pamoja na wadaiwa sugu waliokuwa wamedhulumu fedha .

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu Mkurugenzi huyo wa TAKUKURU amesema Taasisi hiyo imekuwa ikijielekeza zaidi kuelimisha zaidi na kuhabarisha umma  dhidi ya athari za rushwa katika uchaguzi ,umuhimu wa kuchagua viongozi bora  ,waadilifu na wenye uzalendo  na umuhimu wa kutokurubuniwa na mtu yeyote .

Sanjari na hayo,Brigedia Jenerali Mbungo amesisitiza sheria na kanuni za uchaguzi mkuu 2020 kutumika kikamilifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa huru na haki na baadhi ya sheria hizo kuwa ni pamoja na sheria ya uchaguzi wa kitaifa  Na.1 ya mwaka 1985,sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11/2007 na sheria ya Gharama za Uchaguzi Na.6 ya Mwaka 2010.


from MPEKUZI

Comments