SGR ni mradi utawanufaisha watanzania wote


Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dar es Salaam
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaotekelezwa na Serikali nchini utawanufaisha watanzania wote moja kwa moja ikiwa ni ajira kwa upande wa reli yenyewe, kilimo, ama biashara hatua inayosaidia kuinua kipato na uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Kwa hatua ya awali mradi unamanufaa makubwa na umetoa ajira kwa Watanzania  asilimia 51 na wageni asilimia 49 tofauti na hapo awali ambapo ilipangwa wataalamu wa ndani wawe asilimia 20 na wataalamu wan je ya nchi wawe asilimia 80.


Hayo yamesemwa na Meneja wa Kipande cha Morogoro Mkakutupora Singida Mhandisi Mteshi Tito kwa wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati wa siku ya pili ya ziara yao ya kutembe mradi huo na kuongeza hatua hiyo ya uwiano huo wa ajira imefikiwa baada ya Watanzania kuonesha uwezo mkubwa wa uelewa kwenye masuala ya reli.


Aidha, mradi huo unaendelea kutoa ajira kwa watanzania katika maeneo yao ambapo unapita ikizingatiwa ni mradi mkubwa unaopitia mikoa mingi inapopita reli kuanzia Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kigoma ambapo unatarajiwa kufika.


Fauka ya hayo mradi pia unatarajiwa kuwa kutoa fursa nyingi za kiuchumi ambapo utasaidia kusafirisha mizigo kwenda nchi jirani zisizo na bandari ikiwemo Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasiaya Kongo na Uganda hatua itakayosaidia kuchochea kukua kwa uchumi wa nchi.


Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Jamila Mbaruku amewapongeza wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa na moyo wa uzalendo wa kuthamini na kuchukua hatua ya kujionea mradi unaotekelezwa na Serikali kwa fedha za ndani.


“Naamini mtakuwa mabalozi na wajumbe wazuri kwa kuwatangazia Watanzania juu ya mradi wetu huu wa reli ya SGR kwa kuwa ninyi ndiyo wizara yenye kuisemea Serikali, mmeuthamini, mmethubutu na mmeweza kutembelea eneo lote inapopita reli yetu kutoka kituo cha Ihumwa Dodoma hadi kituo kikuu eneo la Posta jijini Dar es Salaam” alisema Jamila. 


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Zahara Nguga amesema kuwa kuna dhana potofu inayoenezwa na watu kuwa mradi huo utawanufaisha wafanyakazi peke yao, la hasha, mradi huo utawanufaisha pia wafanyabiashara na wakulima kutoka maeneo mbalimbali inapopita reli hiyo.


“Hata wakulima, mtu anaweze kuwekeza Kilosa akatoka Dar es salaam saa 11 asubuhi na saa 1 yupo Kilosa akisimamia mifugo, mashamba na mazao yake na jioni anarudi Dar es Salaam kuimarisha maisha yake ya ndoa. Huu ni mradi unawanufaisha watanzania wote” alisisitiza Mkurugenzi Msaidizi huyo.


Wakitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo, Mkuu wa Idara ya Sera na Mipango Petro Lyatuu pamoja na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Leah Kihimbi wamesema kuwa waliazimia kutembelea mradi huo kwa kuzingatia wizara yao ndiyo yenye dhamana ya habari na mradi huo hauna budi kutangazwa na vyombo vya habari ili kuwaelimisha na kuwapa uelewa wananchi juu ya miradi inayotekelezwa na nchi yao.


Lengo la ziara yao la kuufahamu mradi huo limefikiwa kwa kuwa wamejionea malighafi zinazotumika kuutekeleza zinatoka hapa nchini  ikiwemo saruji na nondo zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania na baada ya kukamilika utakuwa na manufaa mengi ikiwemo matumizi mazuri ya muda wa kusafiri ambapo muda wa kusafiri kutoka Dodoma  hadi Dar es salaam utakuwa ni saa tatu na Morogoro hadi Dar es Salaam itakuwa ni dakika 90 sawa na saa 1:30.


Aidha, wameongeza kuwa wamepanda treni inayotumia umeme inayotumiwa na wahandisi kutekeleza majukumu yao na kusema ukiwa ndani ya treni hiyo unaweza kuendelea kufanya kazi za ofisini bila kuwa na mtikisiko wowote na kuongeza kuwa mradi umekuja umejali maisha ya watu kwa maana watautumia na Shirika la Reli limejali vitu vya asili vya kuitamaduni ikiwemo mito na miti ambayo wameitunza vizuri.




from MPEKUZI

Comments