Akitoa tathmini ya mwenendo wa kampeni za chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho kimeendelea na kampeni za kistaarabu na kitapata ushindi wa kishindo mwaka huu.
Kauli yake imekuja siku chache baada ya CHADEMA na ACT Wazalendo kuonesha nia ya kutaka kushirikiana katika ngazi ya Urais, jambo ambalo limepokelewa kwa mitazamo tofauti na wananchi.
“Mimi natoa rai wasisubiri Oktoba 3 ili waungane, hawa waungane sasa halafu ndiyo watajua tulipotoka na tulipofika na Watanzania, sisi tumeingia nchi hii ni maskini huyu mzee Magufuli kapambana leo sisi ni nchi ya uchumi wa kati
“Yule mgombea wa chama cha bwana Zitto kule Zanzibar tutamshinda katika namna ambayo watu wake wa karibu wakae naye karibu, kwa sababu ushindi wa kipindi hiki utakuwa ni mkubwa mno kiasi kwamba wakae karibu kumtia moyo"-Polepole
Mbali na hilo amewataka Watanzania kupuunza baadhi ya hoja ambazo amesema si za ukweli zinazoenezwa na wagombea wa upinzani ikiwemo madai kuwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) haikaguliwa matumizi yake, ununuzi wa ndege ulikuwa nje ya bajeti na kwamba viwanja vya ndege vinajengwa kwa kuangalia maeneo walimotoka viongozi.
Akitolea mfano Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Polepole amesema “… haukujengwa kwa sababu ya Mizengo Kayanza Peter Pinda. Wengi wanaotumia uwanja huo ni watalii wanaokwenda Mbuga ya Wanyama ya Katavi.”
Ameongeza kuwa, kwa tathmini ya CCM, endapo Watanzania wangepiga kura Jumatano (Septemba 23, 2020), mgombea Urais wa chama hicho, Dkt. Magufuli angepata kura asilimia 89.5 ya kura zote halali.
“Kama Watanzania wangepiga kura Jumatano iliyopita, Septemba 23 mwaka huu, mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi, Dkt. Magufuli angeshinda kwa asilimia 89.5"
Kuhusu madai kuwa Dkt. Magufuli anatumia mamlaka ya Urais kwenye kampeni, Polepole amesema kuwa licha ya kuwa kampeni zinaendelea lakini serikali bado ipo kazini na kwamba Rais anakoma kushika wadhifa huo pale mwingine anapoapishwa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment