CCM Waahidi kutoa kivuko kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa kivuko kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.
Ahadi hiyo imetolewa jana (Ijumaa, Septemba 25, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika kitongoji cha Gana.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Majaliwa alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Ukerewe kupitia tiketi ya CCM, Bw. Joseph Mkundi na madiwani. Pia Majaliwa aliwataka wananchi wa Gana wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao wa urais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Akitoa ahadi hiyo mbele ya wananchi wa kisiwa cha Gana, Majaliwa alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 yenye kurasa 303. Kivuko hicho kitatoa huduma kati ya Kakuru na Gana.
Alisema Ilani ya CCM imetoa maelekezo kwa Serikali ijayo itekeleze idadi kubwa ya miradi ya kimkakati ikiwemo kuboresha usafiri wa majini ili kuwandolea adha wananchi wanaoishi katika maeneo ya visiwani.
Majaliwa alisema wananchi zaidi ya 3000 wa Gana, wanahitaji kivuko bora ambacho kitatoa fursa kwao kufanya shughuli za uvuvi na biashara ili kujipatia kipato.
"Hapa Gana tutaleta kivuko, hiki kisiwa ni kikubwa kina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma bora ya usafiri wa majini. Serikali yenu imeweka mipango mizuri kwa ajili yenu," alisema Mheshimiwa Majaliwa.
Alisema Chama kitaendelea kutekeleza Ilani yake kwa vitendo kwa kuboresha huduma za wananchi katika visiwa vyote nchini ikiwemo wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza yenye visiwa 38.
Mbali na kutoa ahadi ya kivuko, Majaliwa alisema Serikali ijayo itapeleka boti za doria kulinda usalama wa wavuvi ambao wakati mwingine wanafanya shughuli zao kwa mashaka wakihofia uvamizi wa majambazi wanaotoka nchi jirani.
Kwa upande wake, Bw. Mkundi alisema kipaumbele cha kwanza baada ya kuingia bungeni ni kuhakikisha Serikali ijayo inaboresha huduma ya afya kwa kujenga idadi kubwa ya zahanati ndani ya kisiwa hicho.
"Gana tuna changamoto ya zahanati, umeme na maji. Nitakuwa daraja zuri kati yenu na Serikali ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia kwa haraka naomba mumchague Rais Magufuli ili mambo yetu yaende vizuri," alisema Bw. Mkundi.
Paschal Bukuru ambaye ni mfanyabiashara ya duka, alisema ujio wa kivuko utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Gana, kwa kuwa muda mrefu wamekuwa wakitumia mitumbwi kwenda Nansio kufuata mahitaji.
Bukuru alisema wafanyabiashara wamekuwa wakipata changamoto ya kuleta bidhaa zao wakitokea Nansio kwa kuwa hawana usafiri wa uhakika, hivyo ujio wa kivuko hicho utakuwa na manufaa makubwa kwao.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM imeahidi kuboresha vivuko ikiwemo ujenzi wa kivuko cha Rugezi-Kisorya (Mwanza). Pia ujenzi wa vivuko vipya vinane utaanza ambao ni Ijinga-Kahangala (Mwanza), Musoma-Kinesi (Mara), Nyamisati-Mafia (Pwani), Msangamkuu-Msemo (Mtwara), Nyakalilo-Kome (Mwanza), Bwiro-Bukondo (Ukerewe), Irugwa-Murutanga (Ukerewe) na Kakuru – Ghana (Ukerewe).
(mwisho)
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment