Wakulima Waiomba Serikali Kuwatafutia Soko La Mazao

Samirah Yusuph, Simiyu.
Baadhi ya wakulima kutoka maeneo mbali mbali hapa nchini wameiomba serikali kupitia  wizara ya kilimo kutafuta soko la mazao wanayozalisha  ili kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ili kufikia malengo ya kulima kilimo  biashara  chenye tija.

Wameyasema hayo jana wakiwa kwenye  mkutano uliowakutanisha wadau wa kilimo kutoka mikoa tofauti nchini  na viongozi wa wilaya za mikoa ya Simiyu, kujadili matumizi ya zana bora za kilimo katika uzalishaji wa mazao mbalimbali kilichofanyika mjini Bariadi.

"uendeshaji wa kilimo biashara unakuwa juu kutokana na zana tunazozitumia huku bidhaa tunazozalisha haziendani , bei ya mazao ipo chini kuliko bei ya zana tunazozitumia hivyo tuiombe serikali hapa nchini kupitia wizara yake ya kilimo kuangalia mfumo mpya masoko yanaendane na ununuzi wa zana" alisema Nkuba Masunga miongoni mwa wakulima waliohudhuria.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alisema kuwa baadhi ya wakulima wameanza kutumia zana bora  za kilimo yakiwemo  matrekta katika uzalishaji ambapo ameongeza kuwa asilimia kubwa ya wananchi mkoani hapo ni wakulima na changamoto kubwa  ni upatikanaji wa vipuli.

"Asilimia 90 ya wananchi wa mkoa wa Simiyu ni wakulima hivyo tunataka kuwa na wakulima wanaopata tija zaidi kwenye shughuli zao za kilimo ambapo niwasitize matumizi ya zana bora za kilimo kwani hakuna mapinduzi ya kilimo bora bila kutumia zana bora pia nitoe rai kwa wadau nje na zana za kupandia na kuvuna ili kuweza kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa "alisema Kiswaga Akimuwakilisha mkuu wa Mkoa wa Simiyu

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Kirasa  inayojihusisha na utoaji wa zana za kilimo Saada Mayuwili ,amewatoa hofu wakulima  juu ya changamoto ya vipuli vya matrekta huku akiongeza kuwa wao wapo kwenye utaratibu wa kufungua maeneo yatakayokuwa yanatoa huduma hizo.

"tumejipanga kuboresha upatikanaji wa vifaa kwa lengo la kuboresha huduma kwa wakulima kwa kuwatambua na kuwasogezea huduma  kwa lengo la kutanua wigo wa kibiashara ili kukuza umoja na ushirikiano wa kibiashara"alisema Mayuwili

Mbali na hilo ameiomba serikali kuona namna ya kuwawezesha kupata eneo ambalo watalitumia kuanda eneo ambalo litakuwa shamba darasa kwaajili ya wakulima huku akiongeza kuwa litakuwa sehemu ya kuongeza tija kwa wakulima.

Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa inayosifika kwa kilimo ambapo mkoa huu unazalisha  mbalimbali  ikiwemo pamba,mpunga, mahindi, na mazao jamii ya mikunde ambapo kupitia mkutano  huo wakulima wamesema licha ya kuletewa huduma ya zana bora bado suala la Soko linaondoa tija katika kilimo.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments